Halmashauri ya Wilaya ya Hanang imeandaa mpango kazi jumuishi wa kuhamasisha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, ukiwaleta pamoja viongozi na wataalamu wa ngazi mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kujiunga na mpango huo kwa ufanisi.
Hatua hiyo imefikiwa katika kikao kazi kilichoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Teresia Irafay, kilichofanyika Februari 12, 2026 katika Ukumbi wa Halmashauri. Kikao hicho kiliwahusisha Wakuu wa Idara (HODs), Maafisa Maendeleo ya Jamii, Maafisa Ustawi wa Jamii, Waganga Wafawidhi, Watendaji wa Kata pamoja na Watendaji wa Vijiji.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Irafay alisisitiza kuwa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ni ajenda ya kimkakati inayohitaji uratibu wa pamoja na uwajibikaji wa kila ngazi ya uongozi. Alieleza kuwa jukumu la kuwafikia wananchi si la sekta ya afya pekee, bali ni la halmashauri kwa ujumla wake, kuanzia ngazi ya wilaya hadi vijijini.

Mratibu wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote Wilaya ya Hanang' Dkt. Peter Marwa akitoa mada katika kikao kazi hicho (Picha Na: Aidan Felson)
Mpango kazi huo umejikita katika kuimarisha utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa bima ya afya, faida zake katika kupunguza gharama za matibabu, na namna ya kujiunga. Aidha, umeweka mkakati wa kufanya mikutano ya hadhara katika kata na vijiji, kutumia watendaji wa mitaa na vijiji kama mabalozi wa uhamasishaji, pamoja na kushirikiana na taasisi za kijamii na viongozi wa dini katika kufikisha ujumbe.
Katika kikao hicho, washiriki walijadili changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa kampeni ya uhamasishaji, ikiwemo uelewa mdogo wa wananchi kuhusu mfumo wa bima, dhana potofu kuhusu gharama na upatikanaji wa huduma, pamoja na umbali wa vituo vya huduma za afya katika baadhi ya maeneo. Mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo iliwekwa wazi, ikiwemo kuandaa ratiba ya ziara za uhamasishaji na kuimarisha utoaji wa taarifa sahihi kupitia mikutano na vyombo vya mawasiliano.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hanang' Mhe. George Bajuta katika kikao kazi hicho (Picha na: Aidan Felson)
Waganga Wafawidhi na Maafisa Maendeleo ya Jamii walikubaliana kushirikiana kwa karibu katika kutoa elimu inayoendana na hali halisi ya maeneo yao, huku Wakuu wa Idara wakiahidi kusimamia utekelezaji wa mpango huo kwa kuzingatia malengo na muda uliopangwa.

Mbunge wa Jimbo La Hanang' Mhe. Asia Halamga akiwa katika kikao kazi (Picha na: Aidan Felson)
Halmashauri imeeleza kuwa utekelezaji wa mpango huu utafuatiliwa kwa karibu kupitia tathmini za mara kwa mara ili kupima mwitikio wa wananchi na kufanya maboresho pale inapobidi. Lengo kuu ni kuhakikisha kila mwananchi wa Hanang anapata fursa ya kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote na kunufaika na huduma za afya kwa uhakika na wakati.
Kupitia mpango huo jumuishi, Halmashauri ya Wilaya ya Hanang imeonesha dhamira ya kuimarisha ustawi wa wananchi wake kwa kuweka afya kuwa kipaumbele cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi



Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.