Halmashauri ya Wilaya ya Hanang mkoani Manyara imeendelea kutekeleza agizo la serikali la utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ambapo kwa mwaka wa fedha 2024/2025 hadi kufikia robo ya tatu, tayari imetoa jumla ya shilingi bilioni 1.5 kwa vikundi vya walengwa hao.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya siku mbili kwa wanufaika wa mikopo hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Hanang, Teresia Irafay, alisema katika kipindi cha robo ya kwanza, halmashauri ilitoa zaidi ya shilingi milioni 800, robo ya pili zaidi ya milioni 500 na robo ya tatu zaidi ya milioni 200.
“Mikopo hii ni sehemu ya jitihada za serikali za kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mapato ya ndani ya halmashauri. Tunahakikisha kuwa vikundi vinapata mafunzo kabla ya kupewa mikopo ili kuhakikisha wanakuwa na uelewa wa matumizi sahihi na umuhimu wa marejesho,” amesema Bi. Irafay.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Hanang’, Mhe. Almish Hazali ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kufunga mafunzo hayo, alimpongeza Mkurugenzi kwa usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato na utekelezaji wa utoaji wa mikopo.
Alisisitiza kuwa mikopo hiyo itumike kwa malengo yaliyokusudiwa badala ya kugawanywa kwa matumizi binafsi. “Nawasihi mfanye kazi kwa bidii na mrejeshe mikopo hii kwa wakati, ili fedha hizi ziweze kuwanufaisha watu wengine pia,” amesema Mhe. Hazali.
Aidha, alivitaka vikundi vyote vinavyopokea mikopo kuzingatia masharti waliyopewa na halmashauri na kuhakikisha wanarudi kutoa mrejesho wa utekelezaji wa miradi yao.
Mpango huu wa utoaji mikopo unalenga kuongeza kipato kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa makundi maalum katika jamii.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.