Wananchi wa Wilaya ya Hanang’ wameanza kunufaika na huduma za kibingwa kutoka kwa timu ya madaktari saba waliobobea, maarufu kama “Madaktari wa Mama Samia”, walioweka kambi ya siku sita wilayani hapa kwa ajili ya kutoa huduma za kitaalamu kwa gharama nafuu.
Akizungumza wakati wa kikao cha mapokezi na utambulisho wa timu hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Hanang Mhe. Almish Hazali alisema kuwa kambi hiyo ya kitabibu ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha huduma za afya zinamfikia kila Mtanzania, bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.
“Huduma hizi ni kwa wananchi wa Hanang’ na hata walioko nje ya wilaya. Madaktari wetu watakuwa hapa kuanzia Juni 1 hadi 7, na tunawakaribisha wote wenye uhitaji kujitokeza,” alisema Mhe. Hazali.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Dkt. Mohammed Kodi, alibainisha kuwa tayari wananchi zaidi ya 200 wamejiandikisha kupata huduma hizo kwa siku ya kwanza pekee, huku akihamasisha jamii kujitokeza kwa wingi.
“Huduma hizi ni za kipekee, zinazotolewa na madaktari bingwa wa fani mbalimbali. Tunawaomba wananchi wachangamkie fursa hii ya kipekee ambayo inaleta unafuu mkubwa kwao,” alisema Dkt. Kodi.
Kambi hiyo ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, ikiwalenga hasa wakazi wa maeneo ya vijijini na pembezoni.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.