Baraza la Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katesh limezinduliwa rasmi leo, tarehe 4 Aprili, 2025 katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Idara ya Kilimo, mjini Katesh, hatua inayolenga kuimarisha usimamizi wa shughuli za kijamii, kiuchumi na kimazingira katika eneo hilo lenye kasi ya ukuaji wa mji.
Katika uzinduzi huo, wajumbe wa Baraza walifanya uchaguzi wa viongozi ambapo Nikomedi Damiano Bayo alichaguliwa kuwa Mwenyekiti, na Isaya Hhayuma Darema kuwa Makamu Mwenyekiti. Viongozi hao watatumikia nafasi hizo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katesh (TEO), Daudi Manda, amesisitiza wajumbe wa baraza kutumia nafasi zao kusimamia kikamilifu sheria ndogo walizozipitisha kwa maslahi ya wananchi.
“Sheria zilizopitishwa ni mwongozo wa matumizi bora ya mji. Tunahitaji mji ulio safi, salama na wenye heshima. Hili halitawezekana kama mifugo itaendelea kuzurura kiholela na mazingira yakabaki machafu,” alieleza Manda kwa msisitizo.
Ameeleza kuwa katika awamu ya kwanza, utekelezaji wa sheria ya kudhibiti mifugo utafanyika katika vitongoji vyote vya Kata ya Katesh na Ganana, kabla ya kupanua wigo huo katika Kata za Jorodom na Dumbeta. Aliongeza kuwa suala la usafi wa mazingira ndio kigezo cha mwisho kilichosalia ili mamlaka hiyo ipate hadhi kamili, hivyo ni lazima lipatiwe uzito unaostahili.
Aidha, Manda alieleza kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katesh inakusudia kuweka mkazo katika maeneo kadhaa ikiwemo kushughulikia migogoro ya ardhi, mipango miji, ukusanyaji wa mapato na usafi wa mazingira, kama mihimili ya maendeleo endelevu ya mji huo na kusisitiza kuwa, ili kufikia lengo hilo, ushirikiano wa karibu kati ya watendaji wa serikali, viongozi wa vitongoji na wananchi ni jambo lisiloepukika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa Baraza hilo, Nikomedi Damiano Bayo, ameapa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria, hasa katika maeneo ya usafi na udhibiti wa mifugo.
“Hatutavumilia tabia ya mifugo kuranda hovyo mitaani wala kuona uchafu ukitawala vitongoji vyetu. Tutachukua hatua kali za kisheria dhidi ya yeyote atakayekiuka sheria, ikiwemo kutozwa faini na kufikishwa mahakamani,” alisema Bayo kwa msimamo thabiti.
Wajumbe wa Baraza hilo nao waliridhia kwa pamoja msisitizo huo na kuahidi kushirikiana katika kuhakikisha kuwa kila eneo linapata mwelekeo thabiti wa usimamizi bora wa ardhi, ukusanyaji mapato, upangaji wa mji na kudumisha usafi kama msingi wa maendeleo na ustawi wa wakazi wa Katesh.
Uzinduzi wa Baraza la Mji Mdogo wa Katesh ni hatua muhimu katika mwelekeo wa kuimarisha mifumo ya utawala wa mji wa Katesh unaokua kwa kasi, katika kusimamia maendeleo, ustawi wa wananchi na utekelezaji wa sera za serikali katika muktadha wa utawala wa karibu na wananchi.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.