Wilaya ya Hanang imetangaza kuwa iko tayari kikamilifu kuwapokea wanafunzi wote wa kidato cha kwanza, darasa la kwanza na elimu ya awali kwa mwaka wa masomo 2026, huku maandalizi yote muhimu ya miundombinu, walimu na mazingira ya kujifunzia yakiwa yamekamilika kabla ya ufunguzi wa shule unaotarajiwa kufanyika Januari 13, 2026.
Kwa upande wa elimu ya sekondari, jumla ya wanafunzi 5,659 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wanatarajiwa kuanza masomo katika shule mbalimbali wilayani hapa ambapo Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari Wilaya ya Hanang, Mwalimu Sophia Msofe, amewahamasisha wazazi na walezi kuhakikisha wanafunzi wote wanaripoti katika shule walizopangiwa bila kuchelewa, akisisitiza kuwa hakuna kikwazo kinachopaswa kuwazuia kuanza masomo kwa wakati.

Amesema serikali inaendelea kutekeleza sera ya elimu bila malipo, hivyo wanafunzi wataruhusiwa kuanza masomo hata kama hawatakuwa na sare za shule katika siku za awali za kuripoti. Ameongeza kuwa walimu na miundombinu ya shule za sekondari iko tayari kuwapokea wanafunzi hao katika shule zote wilayani Hanang.
Wakati huohuo, kwa upande wa elimu ya msingi, Halmashauri ya Wilaya ya Hanang imeeleza kuwa maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa darasa la kwanza na elimu ya awali pia yamekamilika. Shule za msingi zimejiandaa kwa kuweka mazingira rafiki kwa watoto wadogo, ikiwemo madarasa, vyoo, walimu na vifaa vya awali vya kujifunzia, ili kuhakikisha watoto wanaanza masomo katika mazingira salama na rafiki.
Afisa Elimu wa Elimu ya Awali na Msingi Wilaya ya Hanang, Geofrey Abayo, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wote walioandikishwa katika darasa la kwanza na awali wanaripoti shule kwa wakati uliopangwa, akibainisha kuwa elimu ya msingi ni nguzo muhimu katika kujenga msingi imara wa elimu na maendeleo ya mtoto.

Kwa ujumla, Wilaya ya Hanang imejipanga kuhakikisha hakuna mtoto anayeachwa nyuma katika haki yake ya kupata elimu, kwa kuweka mazingira wezeshi ya ujifunzaji katika ngazi zote za elimu ya awali, msingi na sekondari, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya elimu jumuishi na endelevu.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.