Halmashauri ya Wilaya ya Hanang kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imetekeleza zoezi la upandaji na ugawaji wa miche ya miti 5,716 katika kata za Katesh, Nangwa na Maeskron, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa wilaya wa kuhifadhi mazingira na kuimarisha uoto wa asili.
Miche hiyo imepandwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo taasisi za umma, eneo la ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Nangwa pamoja na kugawiwa kwa kaya za wananchi kwa ajili ya kupandwa katika makazi yao, ili kuhakikisha ushiriki wa jamii katika utunzaji wa mazingira unaimarishwa kuanzia ngazi ya kaya.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Bi. Beatrice Ndanu, amesema kuwa zoezi hilo lina lengo la kulinda mazingira, kuboresha hali ya hewa na kuhifadhi vyanzo vya maji kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

“Upandaji wa miche hii ni sehemu ya mkakati mpana wa Wilaya ya Hanang wa kupanda miti na kutunza visiki hai, kwa lengo la kufikia miti 1,500,000 katika kata zote 33. Tunahamasisha wananchi kuhakikisha miti yote iliyopandwa inatunzwa ili ifikie hatua ya kukua na kuleta tija iliyokusudiwa,” amesema Ndanu.
Ameongeza kuwa, pamoja na upandaji wa miche mipya, wilaya inaendelea kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa jamii kwa kusisitiza umuhimu wa kulinda miti iliyopo na kutunza visiki hai, kama njia ya haraka na endelevu ya kurejesha uoto wa asili.


Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Nangwa amewapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi hilo na kuonesha utayari wao wa kushirikiana na serikali katika kuhifadhi mazingira.
“Ushiriki wa wananchi katika zoezi hili unaonesha uelewa na dhamira ya kulinda mazingira yetu. Tunatoa wito kwa kila mwananchi kuhakikisha miti hii inatunzwa, kwani mazingira bora ni msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” amesema Diwani huyo.
Zoezi hilo ni sehemu ya kampeni endelevu ya utunzaji wa mazingira inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Hanang kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha vyanzo vya maji na kuhakikisha wilaya inakuwa na mazingira safi na salama kwa ustawi wa jamii.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.