Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara imeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ baada ya kufanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali Mei 13, 2025.
Ziara hiyo, iliyoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, Peter Toima, ilihusisha ukaguzi wa miradi saba ya maendeleo. Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa Shule ya Msingi Queen Sendiga katika kijiji cha Waret, Shule ya Sekondari Dawar, stendi mpya ya mabasi Katesh, wodi ya wazazi katika Hospitali ya Wilaya ya Hanang’ (Tumaini), mradi wa umeme kijiji cha Dumbeta, na mradi wa maji kijiji cha Bassutughang.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Toima alisema kamati imeridhika na hatua ya utekelezaji wa miradi na kuipongeza menejimenti ya Halmashauri kwa usimamizi mzuri.
"Miradi yote tuliyotembelea ina thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 12, na tumeridhika na ubora wa kazi pamoja na jinsi inavyotekelezwa kwa kuzingatia thamani ya fedha. Halmashauri ya Hanang’ inapaswa kupongezwa kwa kazi nzuri," alisema Toima.
Kamati hiyo imetoa wito kwa watendaji wa Halmashauri kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hadi kukamilika kwake, ili wananchi wanufaike na huduma zinazotarajiwa.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, amesema stendi ya kisasa ya mabasi ya Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyopo Hanang’ itaanza kazi mwishoni mwa Juni mwaka huu. Alitoa kauli hiyo wakati wa ziara ya kamati hiyo ya siasa, baada ya kukagua mradi huo.
Katika ziara hiyo, Kamati ya Siasa pia ilitembelea ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Dawar, ambapo Toima alieleza kuridhishwa na hatua ya ujenzi iliyofikiwa. Awali, Mhe. Sendiga aliwasilisha taarifa kwa niaba ya Serikali na kusema kuwa kutokana na usimamizi mzuri, shule hiyo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Juni.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’, Teresia Irafay, amekuwa akisisitiza wataalamu kuhakikisha ubora wa miradi yote inayotekelezwa, huku menejimenti ikijipangia kuhakikisha miradi mipya na viporo inakamilika kwa wakati.
Shule ya Msingi Queen Sendiga, iliyopo kitongoji cha Waret, ilivutia kamati hiyo kutokana na ubora wa ujenzi. Toima alisema kukamilika kwake na kuanza kupokea wanafunzi ni faraja kwa wahanga wa maporomoko ya tope waliopatiwa makazi 109 na Serikali katika eneo hilo.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.