Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Mheshimiwa Almish Hazali, ameagiza shule zote za msingi na sekondari wilayani humo kuhakikisha zinatoa chakula cha mchana kwa wanafunzi wote. Agizo hilo limetolewa wakati wa kikao maalum kilichojadili hali ya lishe na mikakati ya kuboresha afya za wanafunzi shuleni.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Mhe. Hazali ameeleza kuwa utoaji wa chakula shuleni ni hatua muhimu katika kupambana na changamoto za lishe duni na kuongeza mahudhurio ya wanafunzi. Ameeleza kuwa lishe bora ni msingi wa maendeleo ya elimu na afya kwa watoto.
“Mnatakiwa kuhakikisha mpango huu unatekelezwa ipasavyo. Watendaji wa kata na vijiji mna jukumu kubwa la kuhamasisha wazazi na wananchi kwa ujumla ili wachangie chakula shuleni. Tunataka kuona watoto wanapata lishe bora na wanaendelea vizuri kielimu,” alisema Mhe. Hazali.
Ameongeza kuwa kwa sasa ni kipindi cha mavuno, hivyo upatikanaji wa chakula ni rahisi zaidi. Amehimiza viongozi na wananchi kutumia fursa hiyo vizuri ili kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekosa chakula shuleni.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Teresia Irafay, ameunga mkono agizo la Mkuu wa Wilaya na kutoa maelekezo kwa Afisa Lishe wa wilaya pamoja na watendaji wote kuhakikisha mpango huo unasimamiwa kwa ufanisi.
Irafay amesema lengo ni kuhakikisha hakuna shule inatoa chakula kwa baadhi ya madarasa pekee, bali kila mwanafunzi anufaike.
“Sitarajii kuona chakula kinatolewa shuleni kwa baadhi ya madarasa tu. Tumieni fursa hii ya msimu wa mavuno kuhamasisha wazazi kuchangia chakula na kuhakikisha lishe bora kwa watoto wetu,” alisema Irafay.
Aidha, amewataka watendaji wa kata na vijiji kushirikiana kwa karibu na kamati za shule pamoja na jamii ili kuweka mipango madhubuti ya ununuzi na upishi wa chakula shuleni kwa njia endelevu.
Mpango huu unalenga kuboresha afya ya wanafunzi, kuongeza kiwango cha mahudhurio na ufaulu, na kusaidia kupunguza utoro shuleni kwa kuhakikisha watoto wanapata mlo kamili wakiwa shuleni.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.