Mkuu wa Wilaya ya Hanang’, Mhe. Almishi Isa Hazali, ameendelea na mikutano yake ya uhamasishaji na uelimishaji kwa viongozi wa vijiji, vitongoji, watendaji, na viongozi wa dini, lengo likiwa ni kuimarisha usalama, maadili, na mshikamano katika jamii ya Hanang’.
Katika kikao cha kwanza kilichowahusisha watendaji na wenyeviti wa vitongoji, elimu ilitolewa kuhusu uhamiaji na ulinzi wa wananchi pamoja na mali zao vijijini.
Afisa Uhamiaji wa Wilaya, Ndugu Albert Buchafwe, aliwakumbusha viongozi hao kuwa na jukumu la kuwatambua na kuwafichua wahamiaji haramu katika maeneo yao, kutokukodisha mashamba au ardhi kwa wageni bila kufuata kanuni na sheria za nchi, na kuhakikisha kila mgeni anasajiliwa mara tu anapowasili.
Aidha, aliwahimiza kuweka daftari la wakazi katika kila kitongoji kwa ajili ya kudhibiti mienendo ya watu na kulinda usalama wa wilaya na taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Mhe. Hazali amekutana na viongozi wa dini mbalimbali wilayani Hanang’, akiwashukuru kwa kazi kubwa wanayoendelea kufanya katika kujenga jamii yenye amani, upendo, na mshikamano.
Amewaomba viongozi hao kuendelea kusimamia maadili ya vijana, kuwaongoza katika njia za uadilifu na uzalendo, pamoja na kuombea taifa na viongozi wake, hususan Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia, Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza umuhimu wa kuanzishwa na kuimarishwa kwa mabaraza ya wazee katika kila kata, akieleza kuwa wazee ni hazina ya hekima na ushauri katika utatuzi wa migogoro na utunzaji wa mila na desturi zinazojenga umoja wa kitaifa.
Kupitia mikutano hiyo, serikali ya wilaya inaendelea kujenga msingi imara wa ushirikiano kati ya serikali, wananchi, na taasisi za dini katika kulinda amani, kuimarisha maadili, na kuhimiza maendeleo endelevu katika Wilaya ya Hanang’.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.