Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang', Teresia Irafay, ametoa wito kwa wananchi kuchukua hatua madhubuti za kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza (NCDs), ambayo yanaongezeka kwa kasi wilayani humo.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya kupiga vita magonjwa hayo, yaliyofanyika leo Novemba 15, 2025 katika viwanja vya Mount Hanang', Irafay aliwapongeza wataalamu wa afya kwa kutoa elimu kwa wananchi zaidi ya 5,600, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kujenga jamii yenye afya bora na uelewa sahihi wa kinga dhidi ya magonjwa haya kimataifa.

Maadhimisho hayo yalihusisha michezo na burudani mbalimbali ikiwemo riadha, soka, volleyball, kukimbiza kuku, pamoja na vipindi vya uelimishaji, ambapo wananchi walishiriki kwa wingi. Irafay alisema matumizi ya michezo na burudani kama njia ya kutoa elimu ni nyenzo muhimu katika kuhamasisha jamii kubadili tabia ili kupunguza hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza, yakiwemo kisukari, shinikizo la damu, saratani na magonjwa ya moyo.
Akiwasilisha taarifa ya hali ya magonjwa hayo, Mratibu wa Magonjwa Yasiyoambukiza Wilaya ya Hanang', Dkt. Catherine Ambrose, alisema kuwa hadi Septemba 2025 jumla ya wagonjwa 6,218 waligunduliwa kuwa na magonjwa yasiyoambukiza, ikilinganishwa na wagonjwa 5,000 mwaka 2024. Alisema ongezeko hilo linaonyesha wazi kuwa bado kuna kazi kubwa ya kuendelea kuelimisha jamii juu ya kinga na mabadiliko ya mtindo wa maisha.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Mohammed Kodi, alisisitiza umuhimu wa wananchi kufanya mazoezi mara kwa mara, kuongeza ulaji wa mboga na matunda, kupunguza vyakula vyenye mafuta mengi, pamoja na kujiepusha na matumizi ya tumbaku na pombe kupita kiasi. Alisema hatua hizo zinaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa vifo vya mapema vinavyosababishwa na magonjwa yasiyoambukiza, ambayo kwa sasa ni moja ya changamoto kubwa za kiafya nchini.
Kwa ujumla, maadhimisho hayo yameendelea kuikumbusha jamii ya Hanang’ umuhimu wa kuchukua hatua za kinga na kubadili tabia ili kujenga kizazi chenye afya bora na kupunguza mzigo wa magonjwa yasiyoambukiza katika jamii.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.