Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Teresia Irafay, amekabidhi vitendea kazi kwa kikosi kazi cha usajili na utambuzi wa maduka yanayouza vyakula na vipodozi wilayani Hanang.
Vitendea kazi hivyo, ambavyo ni vishkwambi 11, vitatumika kurahisisha na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kikosi kazi hicho, ikiwemo usajili wa maduka, ukusanyaji wa taarifa muhimu na ufuatiliaji wa ubora wa bidhaa zinazouzwa kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Irafay alisema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Halmashauri kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana karibu zaidi na wananchi, sambamba na kusimamia kwa karibu ubora na usalama wa bidhaa zinazotumika majumbani na katika jamii kwa ujumla.
“Kupitia vitendea kazi hivi, tunataka kuhakikisha usajili wa maduka na ufuatiliaji wa bidhaa unafanyika kwa wakati na kwa ufanisi. Wananchi wanapaswa kuwa na uhakika kwamba bidhaa wanazonunua zina ubora unaokubalika na salama kwa matumizi,” alisema Irafay.
Hatua hii imekuja kufuatia uamuzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kurasimisha na kuhamishia baadhi ya majukumu yake ya usajili wa vyakula na vipodozi katika halmashauri za wilaya, ili kusogeza huduma hizo karibu zaidi na wananchi na kupunguza gharama na usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.
Kwa mujibu wa TBS, mpango huo wa kurasimisha majukumu katika ngazi ya halmashauri unalenga kuongeza kasi ya udhibiti wa ubora wa bidhaa, kuwajengea wajasiriamali wadogo mazingira rafiki ya kufanya biashara zao kwa kufuata viwango, pamoja na kuongeza mapato ya halmashauri kupitia ada na tozo za usajili.
Aidha, wananchi wamehimizwa kushirikiana na kikosi kazi hicho kwa kutoa ushirikiano na taarifa pale inapobainika uwepo wa bidhaa hafifu au zisizo salama katika soko, ili kulinda afya za watumiaji na kuimarisha uchumi wa wilaya.
Kwa upande wake, kikosi kazi hicho kimeahidi kutumia vitendea kazi hivyo kwa ufanisi mkubwa, huku kikiwa na azma ya kuhakikisha Hanang inakuwa mfano bora katika utekelezaji wa mpango huo wa TBS.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.