Halmashauri ya Wilaya ya Hanang imeendelea kusimamia utekelezaji wa zoezi la usafi wa mazingira kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi katika maeneo ya taasisi za umma na makazi ya wananchi ambapo leo usafi unafanyika katika maeneo mbalimbali.
Katika maeneo ya mamlaka ya mji Mdogo wa Katesh, Afisa Mtendaji mkuu wa mamlaka hiyo Daudi Manda Darabe amewaongoza wakazi kufanya usafi katika maeneo ya biashara ya maeneo ya umma huku akisisitiza kuwa zoezi hilo litaendelea mara mbili kila wiki katika eneo lote la mamlaka ya mji Mdogo.
Afisa Mtendaji Mkuu (TEO) wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katesh, Daudi Manda Darabe akihamasisha wafanyabiashara katika eneo la stendi ya mabasi ya Katesh kushiriki zoezi la usafi.
Manda amewataka wafanyabiashara na wakazi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katesh kutoa ushirikiano kwa wasimamizi wa usafi huku akitangaza marufuku ya kutupa taka ovyo ambayo itaambatana na faini ya shilingi elfu 50.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti wa Taka Ngumu na Usafi wa Mazingira katika Wilaya ya Hanang, Ayoub Semdumbe, ameongoza kampeni ya usafi kwa kaya katika kitongoji cha Waret, akisisitiza umuhimu wa mazingira safi na salama.
Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti wa Taka Ngumu na Usafi wa Mazingira katika Wilaya ya Hanang, Ayoub Semdumbe,akihamasisha kampeni ya usafi kwa kaya katika kitongoji cha Waret.
Akizungumza na wakazi wa eneo hilo, Semdumbe amewataka wananchi kuhakikisha wanazingatia kanuni za usafi, ikiwemo kufyeka nyasi zinazozunguka makazi yao ili kudhibiti mazalia ya mbu.
Kwingineko katika vijiji mbalimbali vya wilaya ya Hanang ikiwemo Laghanga wananchi wameipongeza serikali kwa jitihada zake za kuelimisha na kuhamasisha jamii kushiriki katika shughuli za usafi.
Hatua hii ni sehemu ya utaratibu wa kawaida wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, inayofanya usafi wa mazingira kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi katika maeneo yote ya wilaya.
Baadhi ya wananchi na Viongozi wa kijiji cha Laghanga katika picha ya pamoja mara baada ya kukamilisha zoezi la usafi wa mazingira katika viunga mbalimbali kijijini hapo
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.