Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ imeendelea kung’ara katika mashindano ya Shirikisho la Michezo la Serikali za Mitaa Tanzania (SHIMISEMITA) yanayoendelea jijini Tanga, baada ya timu zake zote mbili za mpira wa wavu (wanaume na wanawake) kutinga hatua ya 16 bora. Mchezo huo uliopigwa mchana wa leo Agosti 23, 2025 katika viwanja vya Tanga School umeibua gumzo kwa mashabiki wa michezo kutokana na ubabe ulioonyeshwa na wanamichezo hao.
Katika mchezo wa awali, timu ya wanawake ya Hanang’ iliibuka na ushindi mnono dhidi ya wapinzani wao kutoka Halmashauri ya Mufindi. Waliweza kushinda kwa seti 2-0, wakifunga alama 25-09 na 25-13. Matokeo haya yaliwaweka kileleni mwa kundi A kwa alama 15, na kuthibitisha nafasi yao katika hatua inayofuata ya mashindano. Ushindi huo uliamsha shangwe kubwa kutoka kwa mashabiki waliokuwa wakifuatilia pambano hilo.
Kwa upande wa wanaume, Hanang’ pia ilionyesha uwezo mkubwa baada ya kuitandika timu ya Rorya DC. Katika mchezo uliokuwa wa ushindani, Hanang’ iliibuka na ushindi wa seti 2-0, kwa alama 25-11 na 25-14. Matokeo haya yamezidi kudhihirisha kwamba timu hiyo iko katika ubora wa hali ya juu na imejipanga ipasavyo kwa hatua zinazofuata.
Kupitia matokeo haya, timu zote mbili za Hanang’ DC sasa zimesonga mbele hadi hatua ya 16 bora, zikisubiri kumalizika kwa michezo kutoka makundi mengine ili kujua wapinzani wao watakaokutana nao. Hatua hii ni ya kihistoria kwa Hanang’ kwani inaonyesha mwelekeo mzuri wa maandalizi na ari kubwa ya watumishi kushiriki michezo kama sehemu ya kujenga mshikamano na afya bora.
Mashabiki na viongozi wa michezo wilayani Hanang’ wameipongeza timu hiyo kwa kuendeleza nidhamu, mshikamo na bidii ambayo imeiwezesha kuendelea kupanda chati katika mashindano haya makubwa ya kitaifa. Wameeleza matumaini makubwa kuwa kwa kasi hii, Hanang’ inaweza kufika mbali zaidi na hata kufikiria kurejea nyumbani na makombe.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.