Timu ya kandanda ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ imeendelea kuonesha makali yake katika mashindano ya SHIMISEMITA yanayoendelea jijini Tanga, baada ya kufuzu hatua ya robo fainali kwa kishindo.
Katika mchezo uliopigwa jioni ya leo kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Galanos, Hanang’ DC iliibuka na ushindi wa mabao 2–0 dhidi ya Mpimbwe DC, ushindi uliotokana na uimara wa kiufundi na umakini wa wachezaji.
Kwa upande wa riadha, Hanang’ imejipatia medali nyingine kupitia mkimbiaji wake Vincent Kanyogoto, aliyeibuka kinara katika mbio za mita 100 na kuendeleza rekodi yake nzuri baada ya kung’ara katika mashindano yaliyopita.
Tayari Hanang’ DC ilikuwa imeshatwaa medali ya kwanza kupitia wachezaji wa kike katika mbio za kupokezana vijiti (relay), hatua inayothibitisha ubora wa timu hiyo katika nyanja mbalimbali za michezo.
Kocha wa timu ya soka, Salim Ally Amri, amesema ushindi huo umetokana na nidhamu na morali ya juu ya wachezaji wake, hali iliyowawezesha kutawala mchezo na kufanikisha ushindi huo.
Kwa upande wake, Afisa Michezo wa Wilaya ya Hanang, Bernad Sambagi, amepongeza jitihada za Mkurugenzi wa Halmashauri, Teresia Irafay. Amesema mchango wake mkubwa katika maandalizi ya timu tangu siku ya kwanza ya mashindano ndio siri ya mafanikio haya.
Hadi kufikia Agosti 25, 2025, Hanang’ DC imesalia kuwa halmashauri pekee kutoka Mkoa wa Manyara inayoendelea kushiriki michezo ya SHIMISEMITA, jambo linaloipa heshima kubwa na kuongeza matarajio ya kutwaa medali zaidi.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.