Wilaya ya Hanang imeadhimisha miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kuchangia damu, upandaji miti na usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Sherehe hizo zilianza kwa mazoezi ya mchakamchaka (jogging) yaliyoandaliwa kwa ajili ya watumishi wa umma na wananchi, yakianzia katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Hanang na kuishia katika eneo la Nangwa, ambapo washiriki walishiriki katika shughuli za usafi wa mazingira katika kijiji cha Nangwa na maeneo ya jirani.
Katika kuendeleza maadhimisho hayo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Hanang, Mwalimu Athuman Likeyekeye, akiwa mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya, aliwaongoza wananchi katika zoezi la upandaji wa miti katika chanzo cha maji kilichopo kijiji cha Qutesh, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji.
Maadhimisho hayo yaliambatana na bonanza maalum la michezo lililofanyika katika viwanja vya Chuo cha Ufundi Stadi Nangwa (VTC), likiwa sehemu ya kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi).
Bonanza hilo liliwaleta pamoja watumishi wa serikali waliopambana katika michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, pete, kikapu, kukimbia kwenye magunia na kuvuta kamba.
Katika ujumbe wake kwa washiriki, Katibu Tawala wa Wilaya alisisitiza umuhimu wa mazoezi katika kuimarisha afya na mshikamano wa kijamii, akihimiza jamii kuendelea na utamaduni huo kwa maendeleo endelevu ya wilaya.
Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yanatarajiwa kufanyika mkoani Singida tarehe 1 Mei 2025.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.