Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ imekusanya zaidi ya shilingi 4,607,953,215.75 katika kipindi cha Julai hadi Novemba 2025 sawa na asilimia 46 ya shilingi 10,009,440,000 inayolengwa kukusanywa kwa mwaka 2025/26 hatua inayotajwa kuongeza uwezo wa Halmashauri kutekeleza miradi ya maendeleo.
Akisoma taarifa ya shughuli za Halmashauri zilizofanyika katika kipindi cha mwezi Julai - Novemba 2025 mbele ya baraza la madiwani, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Teresia Irafay, amesema makusanyo hayo yamewezesha Halmashauri kuendelea na miradi mikubwa katika sekta za afya, elimu na kilimo.
DED Irafay amewaeleza madiwani kuwa fedha za maendeleo zilizopokelewa katika kipindi hicho zimefikia shilingi bilioni 3.3 kutoka serikali kuu, mapato ya ndani na wahisani na sehemu kubwa ya fedha hizo inaendelea kutumika katika ujenzi wa shule mpya, kukamilisha maabara, madarasa na maktaba katika shule zaidi ya kumi na tano, pamoja na ujenzi wa vituo vipya vya afya. Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa Kituo cha Afya Hidet chenye thamani ya shilingi milioni 250 na kukamilisha zahanati kadhaa zikiwemo za Garbap, Gabadaw na Gawidu.
Katika sekta ya mifugo, Halmashauri imetekeleza kampeni ya chanjo kwa wanyama ambapo zaidi ya ng’ombe 83,000 wamechanjwa dhidi ya homa ya mapafu, huku mbuzi na kondoo zaidi ya 31,000 wakipatiwa chanjo ya sotoka. Zaidi ya kuku 460,000 pia walichanjwa dhidi ya magonjwa ya kideri, gumboro na ndui. Taarifa hiyo imeeleza kuwa mashamba ya Halmashauri ya Gawal na Bassotu yameingiza zaidi ya shilingi milioni 984 kutokana na ukodishaji, hatua inayochangia mapato ya ndani ya wilaya.
Huduma za afya zimeendelea kuimarika ambapo vituo 37 kati ya 42 vinatoa chanjo kwa ufanisi wa asilimia 100 ambapo taarifa hiyo imesema jumla ya chupa 186 za damu zimekusanywa sawa na asilimia 101 ya lengo, huku watu zaidi ya 4,300 wakipimwa VVU na 38 kubainika kuwa na maambukizi. Huduma kwa wagonjwa wa VVU zimeendelea kutolewa katika vituo vya tiba na matunzo, ambako zaidi ya watu 1,600 wanahudumiwa.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa Halmashauri imeendelea kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo ya makundi maalum, ambapo zaidi ya shilingi milioni 500 zimetengwa kwa ajili ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Vikundi vilivyokopeshwa katika awamu iliyopita vimerudisha zaidi ya shilingi milioni 122 katika kipindi hicho.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.