Halmashauri ya Wilaya ya Hanang imeongeza nguvu katika maboresho ya lishe kupitia maamuzi muhimu yaliyofikiwa katika kikao cha Kamati ya Lishe ya Wilaya kilichofanyika mjini Katesh. Katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Mhe. Almishi Hazali, kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Teresia Irafay, alitoa agizo kwa shule 54 za msingi ambazo bado hazitoi chakula cha mchana kuhakikisha zinaanza kutoa huduma hiyo ifikapo Januari 2026. Amesisitiza kuwa lishe shuleni ni msingi wa afya bora kwa wanafunzi na ni nguzo muhimu katika kuinua kiwango cha ufaulu.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Irafay alizipongeza shule 95 kati ya 149 za msingi ambazo tayari zinatoa chakula cha mchana, sawa na asilimia 64. Hata hivyo, alisisitiza kuwa bado kuna kazi kubwa ya kuhakikisha shule zote zinatoa huduma hiyo. Aidha, amekemea imani potofu zinazowafanya baadhi ya wazazi kukataa kuchangia chakula kwa kisingizio cha kuwatunza watoto dhidi ya “kurogwa”, akisema mitazamo hiyo inarudisha nyuma juhudi za kuboresha elimu na afya za wanafunzi.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Irafay aliongoza majadiliano na wadau mbalimbali kujadili hali ya utekelezaji wa mpango wa lishe wilayani Hanang yaliyolenga kutathmini changamoto zilizopo, kuweka mikakati mipya, na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, viongozi wa vijiji, wataalamu wa afya na jamii ili kuhakikisha mpango wa lishe unatekelezwa kwa ufanisi.
Taarifa ya robo ya kwanza ya mwaka 2025/2026 iliyowasilishwa na Afisa Lishe wa Wilaya, Blandina Kapongo, imeonyesha hatua kubwa katika utekelezaji wa Mkataba wa Lishe. Kapongo ameeleza kuwa asilimia 77.8 ya akinamama na walezi wenye watoto chini ya miaka miwili, ambayo ni sawa na 28,229 kati ya 29,752 waliolengwa, wamepatiwa elimu ya lishe.

Aidha, kumekuwa na ongezeko la asilimia tano la wanawake wajawazito wanaohudhuria kliniki kabla ya wiki ya 12, kutoka asilimia 43 hadi 48. Katika eneo la afya ya mama, kiwango cha upungufu mkubwa wa damu kwa wajawazito kimeshuka hadi asilimia 1.5, chini ya wastani wa Mkoa wa Manyara ambao upo kwenye asilimia 3.5.
Tathmini hiyo pia imebainisha kuwa watoto watano waliogundulika kuwa na utapiamlo mkali wametibiwa na kupona kikamilifu. Utoaji wa elimu ya lishe umeendelea kufanyika katika shule, mikutano mbalimbali ya vijiji, pamoja na maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Maziwa ya Mama Duniani, hatua inayoonesha dhamira ya wilaya kuboresha ustawi wa wananchi wake.
Kwa ujumla, kikao hicho kimeonyesha mwamko mpya wa serikali ya wilaya na wadau wake katika kuhakikisha kila mtoto na familia ya Hanang wanapata lishe bora, huku upatikanaji wa chakula cha mchana shuleni ukiendelea kupewa kipaumbele cha pekee katika mpango wa maendeleo ya elimu na afya.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.