Wilaya ya Hanang imezindua rasmi zoezi la hamasa ya uchanjaji wa mifugo leo Julai 24, 2025, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa miaka mitano wa serikali wa udhibiti wa magonjwa sumbufu kwa mifugo, unaotarajiwa kutekelezwa kuanzia mwaka wa fedha 2024/25 hadi 2028/29.
Zoezi hilo limezinduliwa na Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Mhe. Almishi Hazali, ambaye ametoa wito kwa wafugaji wote wilayani humo kushiriki kikamilifu ili kuhakikisha mifugo inalindwa na afya ya mifugo inaboreka.
"Ninawasihi wafugaji wote wa Hanang kushirikiana kwa karibu na wataalamu wa mifugo. Zoezi hili si la serikali peke yake bali ni la kwetu sote kwa maslahi ya kiuchumi ya jamii yetu" alisema Mhe. Hazali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Teresia Irafay, amesema kuwa serikali imedhamiria kupunguza gharama za chanjo kwa wafugaji kwa kutoa ruzuku ya moja kwa moja.
"Kwa chanjo ya kuku, serikali imetoa ruzuku ya asilimia 100 hivyo wafugaji hawatalipia chochote. Kwa upande wa ng’ombe, mbuzi na kondoo, wafugaji watalipia nusu ya gharama. Mfano, badala ya shilingi 1,000 kwa chanjo ya ng’ombe, sasa watalipa shilingi 500 tu. Kwa mbuzi na kondoo, gharama ni shilingi 300 badala ya 600” alisema Irafay.
Naye Mkuu wa Divisheni ya Kilimo na Mifugo wa Wilaya hiyo, Daniel Luther, amesema kuwa jumla ya dozi 1,080,000 za chanjo zimepokelewa kwa ajili ya zoezi hilo, zikiwa ni hatua muhimu katika kukabiliana na milipuko ya magonjwa ya mifugo.
"Dozi zilizopokelewa ni pamoja na chanjo 210,000 dhidi ya homa ya mapafu kwa ng’ombe, chanjo 400,000 za ugonjwa wa sotoka kwa mbuzi na kondoo, na dozi 470,000 za ugonjwa wa kideri na gumboro kwa kuku" alisema Luther.
Zoezi hili linatarajiwa kuongeza tija katika sekta ya ufugaji, kupunguza vifo vya mifugo, na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wafugaji wa Wilaya ya Hanang, hasa ikizingatiwa kuwa mifugo ni chanzo kikuu cha kipato kwa wakazi wa eneo hilo.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.