Katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja mwaka 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’, Teresia Irafay, ametoa wito kwa watumishi wa umma kuhakikisha wanatoa huduma bora, zenye heshima na kwa wakati kwa wananchi wote wanaozifikia ofisi za umma.
Akizungumza leo katika hafla fupi ya uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja, iliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri mjini Katesh, Irafay alisema wiki hiyo ni fursa muhimu kwa watumishi kutathmini namna wanavyowahudumia wananchi na kuboresha maeneo yenye changamoto ili kuongeza ufanisi.
“Tuwahudumie wananchi kwa upendo, uwajibikaji na ubunifu. Wananchi ni wateja wetu wakubwa na ni sababu ya sisi kuwepo kazini. Ni jukumu letu kuhakikisha wanapata huduma bora na zenye kuleta matumaini,” alisema Irafay.
Amesisitiza kuwa utoaji wa huduma bora ni kipimo halisi cha uadilifu na uwajibikaji wa mtumishi wa umma, akiwataka viongozi wa idara na vitengo kuhakikisha wanakuwa mfano wa kuigwa katika taaluma na mwenendo wao wa kazi.
Aidha, Irafay alibainisha kuwa halmashauri inaendelea kuboresha mifumo ya utoaji huduma, ikiwemo matumizi ya TEHAMA, ushirikishwaji wa wananchi katika maamuzi na uwazi wa taarifa za umma, ili kuhakikisha huduma zinatolewa kwa haraka na kwa usahihi.
Katika hafla hiyo, watumishi wa idara mbalimbali walishiriki kupitia kaulimbiu ya kitaifa isemayo “Huduma Bora kwa Wateja Ndiyo Uzalendo”, ikisisitiza umuhimu wa kuwahudumia wananchi kwa moyo wa kizalendo na uadilifu.
Kwa upande wake, Mariam Paulo, mkazi wa Katesh, aliyeshiriki hafla hiyo, alipongeza hatua hiyo akisema wiki ya huduma kwa wateja inawapa wananchi nafasi ya kutoa maoni na kusikilizwa moja kwa moja na viongozi wa halmashauri.
“Tunafurahia kuona viongozi wetu wanatupa nafasi ya kueleza changamoto zetu. Hii ni hatua nzuri inayojenga uhusiano mzuri kati ya serikali na wananchi,” alisema Mariam.
Wiki ya Huduma kwa Wateja imeendelea kwa shughuli mbalimbali za kuelimisha wananchi, kupokea maoni, kutoa huduma kwa vitendo, na kutambua watumishi waliofanya vizuri katika utoaji wa huduma.
Kwa mujibu wa Irafay, halmashauri itaendelea kuweka msisitizo kwenye utoaji wa huduma bora kwa wananchi katika mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwemo kuboresha miundombinu ya ofisi, kuongeza uwajibikaji, na kuimarisha maadili ya watumishi wa umma
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.