Mradi wa ujenzi wa jengo la wodi ya wazazi katika Hospitali ya Wilaya ya Hanang (Tumaini), unaotarajiwa kuongeza huduma bora za afya ya mama na mtoto kwa wakazi wa Wilaya ya Hanang’ na maeneo jirani, sasa umefikia asilimia 93 ya utekelezaji.
Mradi huu mkubwa, unaogharimu zaidi ya shilingi milioni 594, umefadhiliwa kupitia fedha za Serikali Kuu na mapato ya ndani ambapo Serikali Kuu imetoa shilingi 560,141,335 huku Halmashauri ikichangia shilingi 34,686,762.28. Msimamizi wa mradi huo Dkt. Peter Marwa amesema, Mkandarasi tayari amelipwa zaidi ya asilimia 90 ya malipo yote na kazi zimesalia kidogo kabla ya makabidhiano rasmi ifikapo Mei 31, 2025.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang Teresia Irafay amesema lengo ni kuboresha maeneo ya kutolea huduma za afya ili kupunguza adha kwa wananchi hususani wajawazito na watoto, ndio maana Serikali imeongeza jengo la wodi ya wazazi katika hospitali hiyo.
Mradi huu unatarajiwa kuwa mkombozi mkubwa kwa akina mama na watoto wachanga kwa kuongeza idadi ya vyumba vya kujifungulia kutoka kimoja hadi vinne, pamoja na kujumuisha chumba cha upasuaji wa dharura ndani ya jengo hilo.
Aidha, idadi ya vitanda imeongezeka kutoka 22 hadi 50, hatua inayotarajiwa kupunguza msongamano na kuboresha utoaji wa huduma kwa wakati.
Kwa upande mwingine, watoto wachanga wanaozaliwa na changamoto za kiafya pia watanufaika kupitia huduma maalumu zitakazotolewa ndani ya jengo hilo jipya.
Wakazi wa Hanang’ sasa wana kila sababu ya kutazamia huduma bora za afya, bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu. Kama alivyonukuliwa mmoja wa viongozi wa hospitali hiyo
Mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya serikali ya kuboresha huduma za afya nchini kwa kuimarisha miundombinu ya hospitali kongwe na kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma stahiki, kwa wakati.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.