Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ leo imefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025, inayoishia mwezi Machi 2025.
Ziara hiyo imeongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mhe. Rose Kamili, na ililenga kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi.
Katika hatua ya awali ya ziara hiyo, Kamati ilitembelea Shule ya Msingi Bomani, ambako inaendelea ujenzi wa shimo la choo kwa ajili ya wanafunzi, mradi unaolenga kuboresha mazingira ya usafi na afya shuleni, hasa katika kipindi hiki ambacho usafi wa mazingira ni kigezo muhimu cha maendeleo ya elimu bora.
Baada ya hapo, wajumbe wa kamati walielekea Shule ya Msingi Katesh B ambako walikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa pamoja na matundu kumi ya vyoo. Mradi huu umeelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada za kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani na kuboresha hali ya kujifunzia kwa watoto.
Kamati hiyo ilieleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi na usimamizi wake, na kutoa wito kwa jamii kuendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi mwingine mkubwa wa ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi ya Dkt. Samia, Mhe. Kamili alisema kuwa stendi hiyo ni kielelezo cha dhamira ya Halmashauri katika kuboresha huduma za usafiri na kuinua uchumi wa wakazi wa Hanang’ na maeneo ya jirani. Stendi hiyo inatarajiwa kuwa kitovu muhimu cha biashara, ajira na usafirishaji katika Wilaya hiyo.
Wajumbe wa kamati walisifu hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa stendi hiyo, wakisema kuwa maendeleo yaliyopo yanaonesha jinsi ambavyo Halmashauri kupitia Mkurugenzi Mtendaji wake imejizatiti kusimamia utekelezaji wa miradi kwa ufanisi.
Aidha, walimpongeza Mkurugenzi kwa kufuatilia kwa karibu hatua zote za utekelezaji na kuonesha uongozi makini unaolenga kuleta matokeo chanya kwa wananchi.
Kwa ujumla, ziara hiyo ya Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango imeonesha kuwa miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Hanang’ inaendelea kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa, huku usimamizi wa karibu kutoka kwa viongozi wa Halmashauri ukitajwa kuwa moja ya sababu za mafanikio hayo.
Kamati imeahidi kuendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi mingine ili kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa manufaa ya wananchi.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.