Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Queen Sendiga, leo amezindua rasmi Kambi Maalumu ya Madaktari Bingwa wa ndani ya mkoa huo katika Hospitali ya Wilaya ya Hanang, Tumaini.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mheshimiwa Sendiga alisema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Madaktari Bingwa wa Ndani ya Mkoa wa Manyara, ambapo kila halmashauri hutenga bajeti ya ndani ili kuwaleta madaktari bingwa kusogeza huduma karibu na wananchi.
“Tunataka kuhakikisha wananchi wote wa Manyara, hata wale walioko maeneo ya mbali, wanapata huduma bora za afya bila kulazimika kusafiri umbali mrefu. Halmashauri ya Hanang’ sasa inakuwa ya tatu kutekeleza mpango huu baada ya halmashauri nyingine mbili kuonesha matokeo chanya,” alisema Mheshimiwa Sendiga.
Mheshimiwa Sendiga aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha mpango huo.
“Serikali imewekeza nguvu kubwa kuboresha huduma za afya nchini. Nitoe rai kwa wananchi kutumia fursa hii ya madaktari bingwa waliopo karibu, kwani huduma hizi kwa kawaida zinapatikana kwa gharama kubwa sana nje ya maeneo yao,” aliongeza Mheshimiwa Sendiga.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Dkt. Mohammed Kodi, alisema lengo la mpango huo ni kupunguza gharama za matibabu na kuongeza upatikanaji wa huduma za kibingwa kwa wananchi.
“Kwa mwaka wa fedha 2024/25, awamu mbili za madaktari bingwa tayari zimefanyika Hanang’ na zaidi ya wananchi 2,400 wamepata huduma za kibingwa, huku watumishi 150 wakijengewa uwezo wa kutoa huduma bora zaidi,” alisema Dkt. Kodi.
Kwa mujibu wa Dkt. Kodi, kambi hiyo ilianza jana na tayari wananchi 300 wamepata huduma. Malengo ni kuhudumia zaidi ya wananchi 1,500 kutoka wilayani Hanang na maeneo ya jirani ndani ya siku tano za kambi hiyo.
Kambi hiyo inatoa huduma za kibingwa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo: Upasuaji, Matibabu ya magonjwa ya ndani (moyo, kisukari na shinikizo la damu), huduma za afya ya wanawake na uzazi, matibabu ya watoto, huduma za macho, pamoja na huduma za masikio, pua, koo na usikivu.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi wa wilaya na mkoa, watumishi wa afya, pamoja na wananchi waliokuwa wakihudumiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Hanang, Tumaini.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.