Katika jitihada za kuboresha huduma za afya ya msingi, Halmashauri ya Wilaya ya Hanang imeanzisha kampeni maalum ya kuhamasisha wananchi kuhusu masuala ya afya ya uzazi, ikilenga kuongeza uelewa na ushiriki wa jamii katika huduma za afya.
Akizungumza katika nyakati tofauti Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Katesh, Dkt. Catherine Ambrose, alisema kampeni hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wanapata elimu muhimu kuhusu kuanza kliniki mapema, umuhimu wa kina mama kuhudhuria kliniki wakiwa na waume zao, pamoja na kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya.
"Tunaamini kuwa ushiriki wa wanaume katika huduma za afya ya uzazi ni jambo muhimu sana. Tunawahamasisha wanandoa kuja pamoja kliniki ili kujenga uelewa wa pamoja na kusaidiana katika safari ya ujauzito hadi kujifungua," alisema Dkt. Catherine.
Mbali na hayo, Dkt. Catherine Ambrose pia alitoa tahadhari juu ya ugonjwa wa M-pox, akiitaka jamii kuwa makini na kuchukua hatua za kujikinga. Aidha, alisisitiza umuhimu wa upimaji wa maambukizi ya virusi vya UKIMWI (VVU) kwa hiari, akihimiza wananchi kujitokeza kwa ajili ya kupima afya zao.
Kampeni hiyo inaendeshwa maeneo mbalimbali katika Halmashauri ya Wilaya Hanang ambapo mpaka sasa tayari Dkt. Catherine akiambatana na timu yake ameyafikia makundi ya wananchi kutoka kijiji cha Jorodom, Kitongoji cha Gwadaat na Kambi ya vijana wa Skauti iliyopo katika shule ya sekondari Dumbeta.
Kampeni hii ni sehemu ya mkakati mpana wa halmashauri kuhakikisha huduma za afya zinawafikia watu wote, hasa vijijini, na kuchangia katika kuboresha ustawi wa jamii ya Hanang.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.