Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mh. Alexander Mnyeti katika ziara yake Wilayani Hanang, ametembelea eneo lenye kusadikiwa kuwepo kwa viashiria vya madini ya Almasi katika Kata ya Bassotu Wilayani Hanang na kuweza kuonana na Viongozi wa Kampuni ya Kudu Resources (TZ) Ltd inayofanya utafiti wa madini hayo katika eneo hilo kwa muda wa miaka 4 hadi hivi sasa.
Kampuni hiyo imekuwa ikilalamikiwa na Wananchi kutoka Kata ya Bassuto hususani kutoka katika maeneo yanayozunguka eneo la utafiti, kuyaona magari ya Kampuni hiyo yakisafirisha udongo/mchanga mwingi pasipo kufahamika mchanga huo unakopelekwa. Aidha Mkuu wa Mkoa Mh. Mnyeti aliitaka Kampuni hiyo kutoa maelezo juu ya udongo/mchanga huo unaosafirishwa.
Katika kutoa majibu hayo, Viongozi wa Kampuni hiyo walitoa maelezo yaliyotofautiana ambapo kabla ya Mkurugenzi wa Kampuni hiyo kuwasili katika eneo la tukio, Mkurugenzi Msaidizi wa Kampuni alipohojiwa alikiri kusafirishwa viroba vya mchanga kama "sample" na Kampuni hiyo kwaajili ya kufanyia utafiti katika Maabara ya Madini iliyoko Jijini Mwanza. Sambamba na hilo Mkurugenzi Msaidizi huyo alieleza kuwa baada ya kufanya upimaji, udongo huo umekuwa ukibaki Maabara ya madini Jijini Mwanza. Aidha alikiri kuthibitika kuwepo kwa madini ya Almasi katika eneo hilo ingawa amedai bado haijathibitika ni kwa kiwango gani.
Baada ya Mkurugenzi mwenyewe wa Kampuni kufika katika eneo hilo maelezo aliyoyatoa yalitofautiana na maelezo ya awali yaliyotolewa na Mkurugenzi Msaidizi. Mkurugenzi huyo amedai kuwa Kampuni imekuwa ikichukua kiasi kidogo sana cha udongo 200g kama "sample" na kupeleka katika maabara Jijini Mwanza kwaajili ya utafiti. Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Kudu Resources ameeleza kuwa Kampuni hiyo hadi sasa haijakamilisha utafiti huo na kudhibitika kuwepo kwa madini hayo. Aidha alidai kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazokwamisha utafiti huo kutokukamilika hadi sasa. Moja ya changamoto alizozitoa ni pamoja na Kampuni kushindwa kufanya kazi vipindi vya mvua, mabadiliko ya Sheria ya madini mwaka 2017, eneo hilo kuwepo kwa Volcani iliyofunika "Grystone Belt" na hivyo utafiti kufanyika kwa ugumu na kuchukua muda mrefu.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mh. Alexander Mnyeti ameigiza Kampuni hiyo kutoa muda wa ukamilishaji wa utafiti huo ambapo Kampuni hiyo inachukua muda mrefu (Miaka 4 hadi sasa) kutoa majibu ya utafiti huo . Aidha Mkuu wa Mkoa ameitaka Kampuni hiyo kufuata Taratibu na Sheria zote za Serikali zinazopaswa kufuatwa, kutosafirisha udongo/mchanga (Sample) pasipo kutaarifu ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Kamishna wa Madini Kanda pamoja na vyombo vya Usalama. Pia ameitaka Kampuni hiyo kutoa majibu ya sample zinazofanyika katika maabara ili Serikali ifahamu pamoja na sample hizo (Udongo/mchanga) kurudishwa baada ya utafiti wa Maabara kukamilika.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara pia amefanikiwa kufanya ziara katika maeneo mengine Wilayani Hanang ambapo ametembela Kiwanda kidogo (Sayuni) kinacho jishughulisha na shughuli mbalimbali ikiwemo uchakataji wa ngozi na utengenezaji wa bidhaa za ngozi(Viatu), Uvunaji wa Asali na usindikaji pamoja na usagaji wa mahindi na upakiaji wa unga kilichopo Kijiji cha Galangala Wilayani Hanang. Mh. Mkuu wa Mkoa amefurahishwa na jitihada za kikundi hicho ambapo ametoa shilingi milioni moja (1,000,000/=) kwaajili ya kuongeza mtaji wa Kikundi hicho. Hata hivyo katika ziara hiyo, Kikundi hicho kimenufaika baada ya kuchangiwa na kupata jumla ya shilingi Milioni nne (4,000,000/=) sambamba na kupewa ahadi ya kufungiwa umeme ndani ya wiki moja ambapo ni agizo la Mkuu wa Mkoa huyo kwa Meneja wa TANESCO Wilaya ya Hanang.
Pia Mkuu wa Mkoa amefanikiwa kutembelea Zahanati ya Galagala na kuweka jiwe la Msingi katika Kituo hicho pamoja na kuongea na wananchi. Aidha Mkuu wa Mkoa wa Manyara amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya kuwaleta watumishi katika Kituo hicho ili Kituo hicho cha Afya kianze kufanyakazi mara moja na Wananchi kuondokana na adha ya kusafiri mwendo mrefu kutafuta huduma ya hosipitali.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mh. Alexander Mnyeti pia ametembelea Kata ya Bassotu na kufanya Mkutano wa Hadhara na Wananchi wa Kijiji cha Bassotu ambapo aliweza kuongea na Wananchi na kusikiliza kero zao mbalimbali.
Baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Bassotu waliojitokeza mbele kwaajili ya kutoa kero zao mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: 0787821459
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.