MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang wameisifu menejimenti ya halmashauri hiyo inayoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Teresia Irafay, kwa namna ilivyotekeleza kwa ufanisi miradi ya maendeleo katika mwaka wa fedha unaoendelea.
Akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani, kilichofanyika leo katika ukumbi wa Halmashauri, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mheshimiwa Rose Kamili, ameeleza kuwa hatua iliyofikiwa ni matokeo ya kazi ya pamoja kati ya menejimenti na uongozi wa Halmashauri.
Hata hivyo, Mheshimiwa Kamili amewataka wataalamu kutoa usaidizi wa karibu na wa haraka kwa wasimamizi wa miradi katika ngazi za vijiji na kata, ili kuepusha miradi viporo na kuhakikisha utekelezaji unafanyika kwa wakati.
"Hatutarajii kuona miradi ikikwama kwa sababu ya ucheleweshaji wa kitaalamu, huu ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha Hanang inasonga mbele bila miradi kusuasua," alisema Mheshimiwa Kamili.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kamili ameagiza madiwani wote kushirikiana kwa karibu na wataalamu katika kata zao kuwahamasisha wanafunzi waliotoroka shule kurejea mara moja akisisitiza kuwa elimu ni msingi wa maendeleo na kwamba kila kiongozi anapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watoto wanapata haki yao ya msingi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Teresia Irafay, pamoja na mambo mengine amewatangazia madiwani kuwa kuanzia Mei 16 hadi 22, 2025, kutafanyika zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili katika wilaya ya Hanang.
"Natoa wito kwa viongozi na wananchi wote kujitokeza kwa wingi ili kuhakikisha kila mwenye sifa anaandikishwa. Hili ni zoezi muhimu kwa maandalizi ya uchaguzi ujao," alisisitiza Irafay.
Aidha Irafay amesema tayari maandalizi ya awali kwa zoezi hilo yameanza, huku halmashauri ikiahidi kutoa ushirikiano kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhakikisha zoezi linafanyika kwa amani na ufanisi.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.