Halmashauri ya Wilaya ya Hanang imefanikiwa kukusanya shilingi 223,467,058 kupitia tozo mbalimbali za minada katika kipindi cha miezi saba, kuanzia Julai 2024 hadi Januari 2025, hili ni ongezeko la asilimia 24.08 ikilinganishwa na makusanyo ya mwaka wa fedha wa 2023/24, ambapo shilingi 180,093,748 zilipatikana kwa mwaka mzima.
Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo limepongeza mafanikio haya, likisisitiza umuhimu wa kubuni mbinu madhubuti za kudhibiti utoroshaji wa mapato yanayotokana na minada na vyanzo vingine vya halmashauri.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Mheshimiwa Rose Kamili, amesema kuwa iwapo mianya ya upotevu wa mapato itazibwa, halmashauri itaweza kukusanya fedha zaidi ambazo zitasaidia kutatua changamoto za wananchi kwa kutekeleza miradi na kuwasogezea huduma kama maji, umeme, barabara na kuboresha sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi.
"Hii ni hatua kubwa kwa halmashauri yetu, tunataka kuona kila shilingi tunayokusanya inatumika ipasavyo katika miradi ya maendeleo na kama tukidhibiti mianya ya upotevu wa mapato, tutaweza kuboresha huduma za afya, elimu na miundombinu kwa wananchi wetu," amesema Mheshimiwa Kamili.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Teresia Irafay, ameahidi kusimamia kwa umakini ukusanyaji wa mapato, huku akiwataka watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha fedha zote zinazokusanywa zinaingizwa kwenye akaunti rasmi ya benki ya halmashauri na si kukaa nazo.
"Tumejipanga kuhakikisha kuwa ukusanyaji wa mapato unakuwa wa uwazi na ufanisi, tunawataka watendaji wote wa vijiji na kata kuwa makini na kuhakikisha kuwa fedha zote zinazokusanywa zinakwenda moja kwa moja katika akaunti rasmi ya halmashauri. Hatutamvumilia yeyote atakayehusika na upotevu wa mapato," amesema Irafay.
Mafanikio haya, ni juhudi za halmashauri katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kuweka mifumo thabiti ya usimamizi wa fedha kwa ajili ya kuboresha ustawi wa jamii ya wananchi wa Hanang.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: 0787821459
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.