Wilaya ya Hanang imeadhimisha ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, Meimosi Aprili 30, 2025 katika viwanja vya Shule ya Msingi Katesh B, ambapo Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Wilaya ya hapa limetoa pongezi kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ kutokana na hatua za makusudi zinazochukuliwa kuwajali watumishi wa umma wa Halmashauri hiyo.
Akizungumza mbele ya hadhira ya mamia ya wafanyakazi waliokusanyika kusherehekea Mei Mosi, Mwenyekiti wa TUCTA wilaya ya Hanang Hanang’, Theofili Ammo, amesema hatua ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Teresia Irafay, kutoa mapema mafao ya likizo kwa watumishi kabla ya mwezi Juni si ya kawaida na ni hatua ya uongozi wa mfano unaostahili kutangazwa kitaifa.
"Tukiwa na uongozi unaoona mbali kama huu wa Hanang’, tunapaswa si tu kusherehekea, bali kuhamasisha halmashauri nyingine nchini kujifunza kutoka hapa. Kwa sasa hatupati malalamiko mengi kutoka kwa watumishi wa Halmashauri yetu, hali hii inazaa utulivu na ari ya kazi kwa watumishi,” amesema Ammo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, uamuzi huo wa mapema wa kuwalipa watumishi fedha zao za likizo umeondoa mkanganyiko na malalamiko ambayo awali yalikuwa yakijitokeza kila mwaka, hasa kipindi cha mwisho wa mwaka wa fedha.
Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Kaimu Mkurugenzi Geoffrey Abayo alipokea pongezi hizo, akiahidi kuziwasilisha kwa Mkurugenzi na kuongeza kuwa utawala wa halmashauri utaendelea kuwekeza katika maslahi ya wafanyakazi kama njia ya kuboresha utoaji huduma kwa jamii.
"Tunaamini kuwa mtumishi mwenye furaha ni msingi wa huduma bora kwa wananchi. Tutaendelea kushughulikia changamoto zinazojitokeza na kuhakikisha mazingira ya kazi yanakuwa rafiki na yenye tija," alieleza Abayo.
Akihitimisha tukio hilo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Hanang’, Mwalimu Athuman Likeyekeye kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, alisisitiza wajibu wa wafanyakazi kuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma bora kwa jamii huku Serikali ikiendelea na maboresho ya mazingira ya kazi.
Siku ya Wafanyakazi Duniani huadhimishwa kote duniani kama siku ya kutafakari na kusherehekea mchango wa wafanyakazi katika ujenzi wa jamii na maendeleo ya taifa.
Maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika kitaifa mkoani Singida Mei 1, 2025 ambapo mgeni rasmi ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.