Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Teresia Irafay, leo Julai 24, 2025, ameongoza kikao cha wadau wa mfumo wa stakabadhi ghalani, kilicholenga kuimarisha maandalizi ya msimu mpya wa ununuzi wa mazao katika wilaya hiyo.
Akizungumza kwenye kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya, Irafay amesema kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa msimu huu umefanyiwa maboresho ili kuondoa changamoto zilizojitokeza katika msimu uliopita, na hivyo kuongeza ufanisi na kuwafikia wakulima wengi zaidi.
"Tumejifunza mengi kutoka msimu uliopita. Kwa msimu huu, tumeongeza vituo vya ukusanyaji kutoka viwili hadi kufikia vituo nane. Hii ni hatua kubwa ya kuhakikisha tunawafikia wakulima wengi vijijini," alisema Irafay.
Ameongeza kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani ukiendeshwa kwa kuzingatia miongozo ya serikali, unaweza kuwa nyenzo madhubuti ya kumkomboa mkulima, kumhakikishia bei nzuri ya mazao na kuongeza usalama wa uhifadhi.
Katika kikao hicho, wadau kutoka taasisi mbalimbali na sekta binafsi walipongeza hatua hizo na kwa pamoja wakasisitiza kuwa mshikamano, uzalendo na ushirikiano kati ya serikali na wadau ndio msingi wa maendeleo ya Hanang’.
"Tunatambua kuwa uzalendo na ushirikiano ndio silaha ya maendeleo. Tukifanya kazi kwa pamoja, wakulima wetu watanufaika zaidi na mfumo huu," alisema mmoja wa washiriki wa kikao hicho.
Kikao hicho kinakuja wakati serikali inaendelea kusisitiza matumizi ya mfumo wa stakabadhi ghalani kama njia ya kuongeza tija kwa mkulima na kudhibiti hasara kutokana na kuuza mazao kwa bei duni.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.