Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, leo Machi 27, 2025 ameendelea na ziara yake ya kikazi wilayani Hanang’, ambapo ametembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo huku akieleza kufurahishwa na mchango mkubwa wa wananchi katika utekelezaji wake.
Akiwa katika Shule ya Sekondari Endasak, Mhe. Sendiga alikagua maendeleo ya ujenzi wa bweni lenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 120, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi. Aidha, ametembelea Shule ya Sekondari Jorojick, ambako wananchi wamechangia Shilingi milioni 42 kwa ajili ya ujenzi wa bweni, huku serikali ikichangia Shilingi milioni 70 ili kukamilisha mradi huo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’, Geofrey Abayo, amethibitisha kuwa tayari serikali imepeleka fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maabara katika Shule ya Sekondari Jorojick, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha miundombinu ya elimu.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Gitting, Mhe. Sendiga amesifu juhudi za wananchi na kueleza kufurahishwa na mshikamano wao katika kuchangia maendeleo ya jamii.
"Nimevutiwa sana na moyo wa wananchi wa Hanang’ hasa kata hii Gitting kujitolea kwa hali na mali. Hii inaonesha dhamira ya dhati ya wananchi kushirikiana na serikali katika kuboresha huduma za kijamii na kuinua maisha ya watu," alisema Mhe. Sendiga.
Aidha, amewapongeza Mtendaji wa Kijiji cha Gitting, Ester Mathew Fissoo, Mtendaji wa Kata Nasra Saidy Kiroboto pamoja na Kaimu Afisa Tarafa Yasinta Sulle, kwa kuhakikisha kuwa mikutano ya hadhara inafanyika mara kwa mara ili kusoma mapato na matumizi ya fedha za umma, akisisitiza kuwa hatua hii inaimarisha uwajibikaji, uaminifu, na ushirikiano kati ya serikali na wananchi.
Amesema Serikali imetenga bajeti katika mwaka wa fedha 2025/26 kwa ajili ya kukamilisha miradi yote kiporo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati na kuwanufaisha wananchi.
Katika kijiji cha Dirma, Mhe. Sendiga aliwahimiza wananchi kuepuka kuchochea migogoro ya mipaka ya vijiji, akisisitiza kuwa migogoro hiyo inapunguza kasi ya maendeleo na kuathiri ustawi wa jamii.
Ziara ya Mkuu wa Mkoa inaendelea, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali za kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: 0787821459
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.