Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, leo Machi 26, 2025 ameanza na ziara yake ya kikazi ya siku 4 wilayani Hanang’ kwa kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kufanya mikutano ya hadhara katika kata ya Laghanga, Ishponga na Gehandu.
Akiwa kijiji cha Muungano, Mhe. Sendiga amekagua ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho, ambapo kukamilika kwa zahanati hiyo kutaboresha huduma za afya kwa wakazi wa kijiji hicho. Aidha, ametembelea ujenzi wa nyumba ya walimu katika Shule ya Sekondari Dkt. Samia na kuridhishwa na hatua mradi ulipofikia, kabla ya kuelekea kata ya Ishponga ambapo alikagua maendeleo ya vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Sekondari Ishponga.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Ishponga, Mkuu wa Mkoa ameahidi kuchangia mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa Kituo cha Afya Ishponga, akisema kuwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za wananchi.
Aidha, amewataka watendaji wa serikali kufanya mikutano ya hadhara mara kwa mara na kusoma mapato na matumizi ili wananchi wafahamu fedha zinazoletwa na serikali zimefanya kitu gani au zinakusudia kutumika katika kazi gani.
Katika hatua nyingine, Mhe. Sendiga ametoa agizo kwa wakazi wa Hanang’ waliofanya shughuli za kilimo kwenye mabonde na vyanzo vya maji kuachia maeneo hayo mara baada ya kuvuna mazao, akisisitiza umuhimu wa kulinda mazingira na vyanzo vya maji kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Ziara hii ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huku akiwahimiza wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika juhudi hizo ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kuleta manufaa kwa jamii.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: 0787821459
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.