Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Queen Sendiga, leo Machi 29, 2025 amehitimisha ziara yake ya siku nne wilayani Hanang, ziara iliyofanyika kuanzia Machi 26, 2025, chini ya kaulimbiu “Sivui Buti Mpaka Kieleweke” ikuwa na lengo la kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Mheshimiwa Sendiga alipata fursa ya kutembelea miradi ya afya, elimu, kilimo, na miundombinu, ambapo alijionea hatua kubwa zilizopigwa katika utekelezaji wa miradi hiyo, uhitimishwa kwa Ziara hiyo ni rasmi sasa Buti limevuka.
Akizungumza katika kikao cha kuhitimisha ziara hiyo, kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri, Mheshimiwa Sendiga ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Hanang kwa jitihada zake katika kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya maendeleo zinatumika ipasavyo.
“Nimefurahishwa na jinsi Halmashauri ya Hanang inavyotenga fedha kwa ajili ya miradi muhimu. Ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa kila senti inayotumika inaleta matokeo chanya kwa wananchi,” alisema Mheshimiwa Sendiga.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa usimamizi thabiti wa rasilimali fedha ili kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa viwango vinavyostahili na kwa wakati. “Ninatoa rai kwa viongozi wa wilaya kuhakikisha miradi yote inasimamiwa kwa uadilifu na uwazi ili kuleta maendeleo kama ilivyo falsafa ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi wote,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Mheshimiwa Almishi Hazali, amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa ziara yake na kwa mwongozo alioutoa, akiahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote ili kuhakikisha maendeleo ya wilaya yanaimarika.
“Ziara hii imetupa dira mpya ya namna bora ya kusimamia miradi yetu. Tutahakikisha tunatekeleza maagizo yote kwa ufanisi ili wananchi wa Hanang waone matunda ya juhudi za serikali yao,” alisema Mheshimiwa Hazali.
Halmashauri ya Wilaya ya Hanang inaendelea kujizatiti katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa ufanisi, ili kuboresha maisha ya wananchi wote wa Hanang na kuleta maendeleo ya kweli katika sekta zote muhimu.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.