Mkuu wa Wilaya ya Hanang’, Mhe. Almishi Isa Hazali, ameendelea na ziara yake ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi, ambapo amefanya mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Muungano na kutembelea shamba la mwekezaji Ngano Ltd lenye zaidi ya ekari 13,000. Shamba hilo ni miongoni mwa mashamba makubwa ya kilimo cha biashara yaliyopo wilayani Hanang’, likiwa na mchango mkubwa katika kuongeza ajira, kipato, na maendeleo ya kijamii.
Katika ziara hiyo, Mhe. Hazali aliambatana na wataalamu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’, wakiwemo Afisa Ardhi na Afisa Sheria, ambao walitoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya umiliki halali wa ardhi, umuhimu wa kuheshimu mipaka, na taratibu za kisheria za uwekezaji. Wananchi pia walipata nafasi ya kueleza changamoto zinazohusiana na matumizi ya ardhi na uhusiano kati yao na wawekezaji wanaofanya shughuli katika maeneo yao.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi na wawekezaji, akibainisha kuwa uwekezaji wa aina hiyo unaleta manufaa makubwa kwa jamii ikiwa kutakuwepo mazingira ya amani, utulivu, na ushirikiano. Aliongeza kuwa migogoro ya ardhi ni moja ya changamoto zinazoweza kuathiri kasi ya maendeleo, hivyo ni wajibu wa viongozi wa kijiji na kata kushirikiana na wataalamu wa ardhi katika kutatua changamoto hizo mapema.

“Ni muhimu wananchi wakatambua kuwa wawekezaji si wapinzani, bali ni wadau wa maendeleo. Tukilinda amani, kuheshimu mipaka na kufuata sheria, wote tutanufaika,” alisema Mhe. Hazali.
Aidha, Mkuu wa Wilaya aliwataka wananchi kuendelea kuwa walinzi wa amani na maendeleo kwa kutumia fursa zinazotolewa na wawekezaji, kama vile ajira, huduma za kijamii, na ushirikiano katika miradi ya kijamii. Pia aliwahimiza viongozi wa vijiji kusimamia vyema matumizi ya ardhi na kuhakikisha wananchi wanapata elimu endelevu kuhusu haki na wajibu wao katika umiliki na matumizi bora ya ardhi.
Mhe. Hazali amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuhimiza uwekezaji unaozingatia sheria na maslahi ya wananchi, sambamba na kuhakikisha wananchi wote wananufaika na shughuli za kiuchumi zinazofanyika katika maeneo yao.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.