Katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na Kwaresma, Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Mheshimiwa Almishi Issa Hazali, ameandaa hafla ya futari nyumbani kwake, ikiunganisha waumini wa Kiislamu pamoja na makundi mbalimbali ya jamii.
Tukio hilo limekuwa fursa ya kujenga uhusiano wa kijamii, kuhimiza mshikamano wa kidini na kijamii, na kufikisha ujumbe muhimu wa maendeleo kwa wananchi.
Mheshimiwa Hazali, akizungumza na wageni waalikwa, aliwashukuru wote waliokubali mwaliko huo na kusisitiza umuhimu wa kutunza akiba ya chakula baada ya mavuno. “Hali ya mazao mwaka huu si ya kuridhisha, hivyo ni muhimu kila familia kuhakikisha inaweka akiba ya chakula cha kutosha kabla ya kuuza mazao yote,” alieleza.
Aidha, alihimiza wazazi kuhakikisha watoto wao wanahudhuria masomo kikamilifu, akisema kuwa Serikali imeboresha mazingira ya elimu ili kila mtoto apate nafasi ya kusoma. “Mzazi ana jukumu kubwa la kuhakikisha mtoto wake anapata elimu bora. Serikali imejenga madarasa, imeleta walimu na vifaa vya kujifunzia, hivyo hakuna sababu ya mtoto kubaki nyumbani,” alisisitiza Mkuu wa Wilaya.
Katika hotuba yake, Sheikh wa Wilaya ya Hanang’, Sheikh Muhdi Said Ronka, amepongeza hatua ya Mkuu wa Wilaya kuandaa hafla hiyo, akibainisha kuwa ni kitendo cha kujenga upendo na kusaidiana.
“Kufuturisha ni ibada kubwa yenye malipo makubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Tunaposhiriki katika matendo haya, tunaimarisha undugu na kuendeleza maadili mema katika jamii,” alisema Sheikh Ronka.
Mmoja wa waumini walioshiriki hafla hiyo, Bi. Amina Juma, alieleza furaha yake kwa tukio hilo, akisema kuwa linasaidia kuimarisha uhusiano kati ya viongozi na wananchi. “Ni jambo jema kuona viongozi wetu wanashiriki nasi katika hafla kama hizi. Inatufanya tujione kuwa sehemu ya jamii yenye mshikamano na amani,” alisema Bi. Amina.
Viongozi wa madhehebu mbalimbali waliokuwepo kwenye hafla hiyo walitumia nafasi hiyo kuwaombea dua viongozi wa wilaya, mkoa na Taifa kwa ujumla, wakisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, hususan kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Tukio hilo limeacha athari chanya kwa jamii, likihamasisha umoja na kuhimiza maadili ya kusaidiana katika nyakati muhimu za kiimani.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: 0787821459
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.