Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Mheshimiwa Almishi Hazali, ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa karakana ya ufundi kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya watu wazima chini ya programu maalumu ya IPOSA.
Hafla hiyo imeenda sambamba na kilele cha maadhimisho ya Juma ya Elimu ya Watu Wazima yaliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Msingi Katesh A.
Akizungumza baada ya hafla hiyo, Mheshimiwa Hazali ameitaka jamii kujitokeza kujiendeleza katika ujuzi mbalimbali kupitia mfumo wa elimu ya watu wazima. Aidha, amewahimiza vijana waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali kujisajili katika kituo hicho ili kujipatia ujuzi utakaowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali.
"Elimu ya watu wazima si kwa wanaoishi mijini pekee, bali kwa kila mkazi wa Hanang. Tunataka kila mtu ajifunze ujuzi utakaomsaidia kujitegemea na kuchangia maendeleo ya wilaya. Vijana waliokatisha masomo, hii ni nafasi yenu ya pili, msiache ipotee”alisema Mheshimiwa Hazali.
Kwa mujibu wa Afisa Elimu ya Watu Wazima wa Wilaya ya Hanang, Lilian Chongolo, hadi sasa kituo hicho kimeandikisha wanafunzi 4 wa fani ya ushonaji na mwanafunzi mmoja wa useremala, huku akitoa wito kwa vijana wengi zaidi kujiunga ili kupata mafunzo hayo muhimu.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Sophia Msofe, amesema Halmashauri imefanikiwa kuwarudisha shuleni wanafunzi 59 wa sekondari waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali chini ya mpango wa Elimu Mbadala ya Sekondari (ASEP) katika vituo viwili, huku jumla ya wanafunzi 60 wakiendelea na masomo ya MEMKWA katika vituo 11.
Ameongeza kuwa juhudi hizo zimechangia kupunguza idadi ya watu wazima wasiojua kusoma na kuandika wilayani Hanang kutoka asilimia 26.6 mwaka 2022 hadi asilimia 18.8 mwaka huu.
Juma la wiki ya elimu ya watu wazima mwaka huu limepambwa na kauli mbiu ya "Kukuza kisomo katika zama za kidigitali kwa maendeleo endelevu ya taifa letu" ikilenga kuchochea matumizi ya zana za kidigitali katika nyanja mbalimbali kwenye jamii
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.