Serikali imekamilisha ujenzi wa nyumba maalum kwa ajili ya kumpatia makazi salama Betrina Basili Francis, binti mwenye mahitaji maalum aliyeathirika vibaya na maporomoko ya tope ya Desemba 2023 yaliyosababisha vifo vya wazazi wake wote. Nyumba hiyo imejengwa katika Kitongoji cha Waret, wilayani Hanang’, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha makundi maalum yanapata huduma na mazingira bora ya kuishi.
Katika ziara ya kukagua mradi huo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, amepongeza hatua kubwa iliyofikiwa na uongozi wa Wilaya ya Hanang’ kwa usimamizi makini hadi kukamilika kwa ujenzi huo kwa asilimia 100.
Dkt. Yonazi amesema:
“Hii ni kazi nzuri na ya kuigwa. Tumejenga nyumba yenye viwango kwa ajili ya mtoto ambaye alipoteza kila kitu. Serikali inaendelea kusimama na watu wenye ulemavu na makundi yaliyo kwenye mazingira hatarishi, na tutahakikisha hawachwi nyuma.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’, Teresia Irafay, ameushukuru uongozi wa mkoa na serikali kuu kwa ushirikiano uliowezesha mradi huo kukamilika kwa wakati. Amesema nyumba hiyo ni matokeo ya nia ya pamoja ya kuhakikisha ustawi wa wananchi, hususan wenye uhitaji maalum.
Irafay amesema “Betrina alikuwa katika mazingira magumu sana baada ya kupoteza wazazi wake. Kukamilika kwa nyumba hii ni uthibitisho kwamba serikali inawajali wananchi wake. Kama halmashauri tutaendelea kumfuatilia na kuhakikisha anapata huduma zote muhimu.”
Nyumba hiyo inatarajiwa kukabidhiwa rasmi kwa Betrina katika siku chache zijazo, hatua itakayompa makazi salama, heshima na mwanzo mpya wa maisha baada ya changamoto nzito alizopitia.



Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.