Wajumbe wa Baraza la Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katesh, Wilaya ya Hanang, wamepatiwa elimu ya kinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa m-pox, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Halmashauri ya Wilaya hiyo kukabiliana na kuenea kwa maradhi hayo.
Akizungumza katika kikao cha uzinduzi wa Baraza la Mamlaka Mji Mdogo Katesh, Daktari kutoka Hospitali ya Wilaya ya Hanang (Tumaini), Catherine Amros, amesema elimu hiyo inalenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu namna ya kujikinga, kutambua dalili na hatua za kuchukua endapo mtu atakuwa na mashaka ya kuambukizwa.
“Tunahimiza ninyi kama wajumbe na wawakilishi wa wananchi kuwa mabalozi wa afya kwa jamii kusambaza ujumbe huu wa tahadhari, hasa katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu ikiwemo mikutano yenu ya vitongoji, na hata katika ngazi ya kaya” alisema Dkt. Amros.
Kwa mujibu wa Dkt. Amros, dalili kuu za m-pox ni pamoja na homa, uchovu, kuvimba tezi, na upele unaojitokeza usoni na sehemu nyingine za mwili, akiongeza kuwa mtu yeyote anayeonesha dalili hizo anapaswa kupelekwa katika kituo cha afya mapema kwa uchunguzi zaidi.
Halmashauri ya Wilaya ya Hanang inaendelea kutoa elimu hiyo kwa makundi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na masoko, shule na taasisi za kidini, ili kuongeza mwamko wa jamii kuhusu kujikinga na ugonjwa huo.
Katika wilaya ya Hanang bado hakuna mlipuko wa m-pox, lakini hatua hizi za kinga ni sehemu ya mkakati wa tahadhari ili kuhakikisha usalama wa wananchi.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.