Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Hanang, imependekeza bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 kufikia Tshs. 2.3 bilioni ili kuboresha miundombinu ya barabara katika wilaya hiyo zenye zaidi ya kilomita 517.
Taarifa hii imetolewa leo na Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Hanang, Eng. Sebastian Tongola katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC), ambapo ameeleza kuwa fedha hizo zitatumika kwa matengenezo ya barabara, ukarabati wa vivuko, pamoja na kushughulikia maeneo korofi yanayokwamisha usafiri wa wananchi wa Hanang.
"Kwa sasa, tunasimamia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 1,050.50, lakini zaidi ya nusu ya barabara hizi ziko katika hali mbaya. Changamoto kubwa ni uharibifu wa miundombinu kutokana na shughuli za binadamu, ikiwa ni pamoja na ujenzi holela na matumizi mabaya ya barabara," amesema Eng. Tongola
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Hanag, Hamad Kaaya akifuatilia maoni ya wajumbe katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC).
Kwa mujibu wa mpango wa TARURA, bajeti hiyo ya Tshs. 2.3 bilioni itatokana na vyanzo mbalimbali vya fedha, ikiwa ni pamoja na Tshs. 829.8 milioni kutoka kwenye Mfuko wa Barabara, Tshs. 500 milioni kutoka katika fedha za Jimbo, na Tshs. 1 bilioni kutoka kwenye tozo ya mafuta.
Matengenezo yanayotarajiwa kufanyika ni pamoja na ukarabati wa kawaida wa barabara kwa Tshs. 128.58 milioni, ambapo zaidi ya 23.56 km za barabara zitaboreshwa. Pia, Tshs. 230 milioni zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa maeneo korofi, huku Tshs. 387 milioni zikielekezwa katika ujenzi wa vivuko 19 katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko na changamoto nyingine za hali ya hewa.
Miongoni mwa barabara zitakazofanyiwa kazi ni pamoja na Balangdalalu - Lalaji (8 km), Endasak - Sabilo (3 km), Gawal - Gawidu (3 km), na Ngalangala - Ghaghata (5 km), ambazo zimekuwa zikisababisha adha kubwa kwa wakazi wa maeneo hayo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Geofrey Abayo akisikiliza kwa umakini hoja za wajumbe.
Licha ya bajeti hiyo kubwa, TARURA inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja na uharibifu wa barabara unaosababishwa na mifugo inayopita kiholela, magari yanayobeba mizigo mizito kupita kiasi, na wananchi wanaotumia sehemu za barabara kwa kilimo na ujenzi holela.
Eng. Tongola ameeleza kuwa TARURA imeweka mkakati wa kuongeza alama za barabarani na kushirikiana na serikali za vijiji kuelimisha wananchi kuhusu matumizi sahihi ya miundombinu.
"Tunawataka wananchi kushirikiana nasi kwa kuheshimu sheria za barabara na kulinda miundombinu ili miradi tunayotekeleza iwe na manufaa ya muda mrefu," amesisitiza.
Wakazi wa Hanang wanasubiri kwa hamu kuona utekelezaji wa bajeti hiyo mpya, huku wakitarajia kwamba uboreshaji wa barabara utarahisisha usafiri na kuinua uchumi wa eneo hilo.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: 0787821459
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.