Ni rekodi iliyoandikwa hii leo na Timu ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ baada ya kuibuka na ushindi wa kishindo katika mashindano ya SHIMISEMITA yanayoendelea jijini Tanga, kwa kushinda michezo yote iliyoshiriki.
Rekodi hii haijafikiwa na timu yoyote katika mashindano haya mwaka huu tangu yaanze Agosti 15 kwa kuibuka na ushindi katika michezo yake yote inayoshiriki.
Katika soka, Hanang’ DC imeichakaza bao 5 kwa nunge (5-0) kibonde wake timu ya Meru DC, mchezo uliopigwa leo mchana katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mzingani, ushindi mnono unaodhihirisha ubora wa kikosi kuanzia ulinzi hadi safu ya ushambuliaji.
Kunako katika mchezo wa wavu (volleyball) upande wa Wanaume, timu ya Hanang’ DC wameichakaza Mbarali DC seti 2–0 (25–10, 25–10), wakitawala mpira wa pili na nidhamu ya uwanjani. Mechi nyingine, Mpimbwe DC waliishia mitini kwa kutotokea katika mchezo hivyo Hanang’ DC ikawekewa ushindi wa mezani wa seti 2–0 (25–0, 25–0) sambamba na pointi 50 za kikanuni.
Kwa upande wa volleyball wanawake, hali ilikuwa vivyo hivyo kama Mpimbwe DC baada ya Kishapu DC kugoma kuingia uwanjani na kuwafanya waamuzi kuipa Hanang’ DC ushindi wa seti 2–0 (25–0, 25–0) na pointi 50.
Riadha nako Hanang' DC haikubaki nyuma, ambapo Joseph Ernest ameshinda mbio za mita 800 na kuingia hatua ya fainali huku Vicent Kanyogoto akishinda mbio za mita 200 na kuingia hatua ya nusu fainali
Kwa ujumla, matokeo ya leo yanaipa Hanang’ DC kasi na ari mpya kwenye mashindano haya, ikionesha kikosi chenye uwiano mzuri katika soka, volleyball na riadha na kuashiria siku zijazo zenye ushindani lakini pia matumaini makubwa ya mataji.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.