WILAYA ya Hanang leo imepokea ujumbe maalum kutoka serikali ya Ethiopia uliokuja kujifunza mbinu za serikali ya Tanzania katika kupambana na majanga ya asili.
Ujumbe huo umeongozwa na Naibu Kamishna wa Kamisheni ya Usimamizi wa Maafa ya Ethiopia (Ethiopia Disaster Risk Management Commission - EDRMC), Bw. Ayderu Hassen, pamoja na wataalamu 15 kutoka Serikali ya Ethiopia na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO-Ethiopia).
Viongozi hao wamepokelewa rasmi na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Mheshimiwa Rose Kamili, kabla ya kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na maporomoko ya tope yaliyotokea Desemba 3, 2023.
Katika ziara hiyo, ujumbe huo umepata fursa ya kujionea ujenzi wa nyumba 109 kwa waathirika wa maafa hayo.
Ujumbe huo kutoka Ethiopia umeipongeza serikali ya Tanzania kwa juhudi zake za haraka katika kushughulikia janga hilo na kurejesha hali ya kawaida kwa muda mfupi. Aidha, wameeleza kufurahishwa na hali ya utulivu waliyoikuta katika maeneo yaliyoathirika.
Ziara hii imedhihirisha umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na changamoto za maafa, huku ikilenga kuimarisha maisha ya watu na kuboresha mifumo ya ustahimilivu kwa nchi zote mbili.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: 0787821459
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.