Katibu Tawala wa Wilaya ya Hanang, Athumani Likeyekeye, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Teresia Irafay, leo wamekutana na maafisa elimu kata, watendaji wa kata na vijiji katika ukumbi wa Halmashauri kwa ajili ya kujadili masuala ya elimu.
Katika kikao hicho, maafisa elimu wametoa taarifa kuhusu hali ya kuripoti kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza, uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali na darasa la kwanza, pamoja na upatikanaji wa chakula shuleni.
Katibu Tawala wa Wilaya, Athumani Likeyekeye, ameagiza kuwa ifikapo Februari 24, 2025, wanafunzi wote wawe wameripoti shuleni, akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wazazi na walezi watakaoshindwa kuhakikisha watoto wao wanahudhuria masomo.
"Serikali imeondoa gharama zote za lazima na imewaruhusu wanafunzi kuanza shule hata kama bado wanavaa sare za shule ya msingi. Hakuna sababu yoyote inayopaswa kuwazuia kuripoti shuleni," alisema Likeyekeye.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Teresia Irafay, amewataka maafisa elimu kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha mchana kwa wanafunzi shuleni, sambamba na kusimamia ukusanyaji wa maduhuli ya serikali.
Aidha, Katibu Tawala amewataka watendaji wa kata na vijiji kusimamia ipasavyo masuala ya ulinzi na usalama katika maeneo yao ili kuhakikisha mazingira bora kwa maendeleo ya elimu wilayani Hanang.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: 0787821459
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.