Katika hatua ya kuimarisha ustawi wa kiuchumi wa jamii, Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ inakusudia kutoa mkopo wa zaidi ya shilingi milioni 799 kwa vikundi 59 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani, ikiwa ni awamu ya pili kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili kwa wanufaika hao yaliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Msingi Katesh A, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Geofrey Abayo, alisema fedha hizo ni utekelezaji wa sera ya Serikali ya Awamu ya Sita ya uwezeshaji kiuchumi kwa makundi maalum.
“Mafanikio haya ni ushahidi wa dhamira ya dhati ya Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwawezesha wananchi wake kiuchumi kupitia mikopo isiyo na riba. Tumehakikisha kuwa vikundi 31 vya wanawake wanapokea shilingi milioni 486.9, vikundi 24 vya vijana vitapata milioni 282.5, na vikundi 4 vya watu wenye ulemavu milioni 29.6,” alisema Abayo.
Mafunzo hayo yanajumuisha masomo ya ujasiriamali, usimamizi wa fedha, mbinu za urejeshaji wa mikopo, na maadili ya uongozi wa vikundi, kwa lengo la kuhakikisha kuwa mikopo hiyo inaleta matokeo chanya kwa jamii nzima ya Hanang’.
William Gaudence, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wilaya ya Hanang', aliwataka wanufaika kutumia vyema mafunzo hayo kama kichocheo cha mabadiliko katika maisha yao ya kiuchumi.
“Lazima tuondokane na dhana ya kuona mikopo hii kama msaada. Hii ni fursa ya kujenga mitaji, kuongeza uzalishaji na kutengeneza ajira. Natoa rai kwa kila kikundi kuhakikisha kinarejesha kwa wakati na kwa mujibu wa makubaliano,” alisema Gaudence.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na halmashauri, mikopo hiyo inatarajiwa kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uzalishaji mali ikiwemo kilimo, ufugaji, biashara ndogo ndogo na huduma za kijamii.
Halmashauri ya Hanang’ imeahidi kuendelea kufuatilia na kutoa mafunzo ya mara kwa mara pamoja na msaada wa kitaalamu ili kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu, yenye mchango halisi katika pato la familia na jamii kwa ujumla.
Hatua hii inatajwa kuwa ni sehemu ya juhudi za kuondoa umasikini wa kipato na kukuza maendeleo ya wananchi wa Hanang’, huku ikisisitizwa kuwa mafanikio ya wanufaika yatafungua milango kwa vikundi vingine zaidi kupata mikopo kama hiyo.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.