Wakulima katika Wilaya ya Hanang’ wamepokea msaada wa lita 2,000 za viuatilifu kwa ajili ya kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao, hatua inayolenga kuimarisha kilimo na kuhakikisha wakulima wanapata mavuno bora.
Mkuu wa Idara ya Kilimo na Mifugo wilaya ya Hanang, Daniel Luther, amesema viuatilifu hivyo vitagawiwa bure kwa wakulima, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuboresha huduma za ugani na kusaidia wakulima wadogo kuhakikisha mazao yao yanakuwa salama dhidi ya wadudu waharibifu.
Akizungumza na wakulima wa kijiji cha Dawar, Luther amewahimiza wakulima kutumia viuatilifu hivyo kwa ufanisi ili kuongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao. Ameeleza kuwa dawa hizo zina uwezo wa kuangamiza wadudu wanaoshambulia mazao mbalimbali shambani, hivyo kupunguza hasara inayosababishwa na wadudu hao.
“Tunawahimiza wakulima kuchukua hatua za haraka kutumia viuatilifu hivi mara tu wanapovipata ili kuhakikisha wanadhibiti wadudu kabla ya kuleta madhara makubwa kwenye mazao yao,” amesema Luther.
Aidha, amewataka maafisa ugani wa kata kuandaa orodha ya wakulima walioko kwenye maeneo yao ili kuhakikisha mgao wa viuatilifu hivyo unawafikia wahitaji wote kwa wakati.
Kwa upande wao, baadhi ya wakulima wa Dawar wameipongeza serikali kwa msaada huo, wakisema utasaidia hasa wale wasio na uwezo wa kununua dawa hizo kwa gharama zao. Wakulima hao wameeleza kuwa upatikanaji wa viuatilifu utaimarisha uzalishaji wa mazao na kusaidia kupunguza upotevu wa mavuno unaotokana na wadudu waharibifu.
Hatua hii ni miongoni mwa jitihada za serikali katika kuboresha sekta ya kilimo, huku ikihamasisha matumizi sahihi ya pembejeo na teknolojia za kisasa kwa wakulima wilayani Hanang.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: 0787821459
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.