Wakulima wa Wilaya ya Hanang wamepata fursa ya kipekee ya kuendeleza kilimo cha kisasa baada ya kukabidhiwa matrekta 20 yaliyotolewa kwa mkopo na Kampuni ya KANU Equipment kwa kushirikiana na Taasisi ya PASS Leasing, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji na kuimarisha matumizi ya teknolojia katika sekta ya kilimo.
Makabidhiano hayo yamefanyika Oktoba 16, 2025, katika hafla iliyofanyika wilayani Hanang’, ambapo Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Mheshimiwa Almishi Hazali, alikuwa mgeni rasmi.
Akizungumza wakati wa kukabidhi matrekta hayo, Mheshimiwa Hazali amesema hatua hiyo ni mwendelezo wa jitihada za serikali za kuhamasisha matumizi ya zana bora za kilimo, kupunguza nguvu kazi ya mikono, na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.
“Tunataka kilimo cha Hanang kiwe cha kisasa, kinachotumia teknolojia na zana bora. Matrekta haya ni mwanzo wa mageuzi tunayoyataka katika kilimo chetu, ili wakulima watumie fursa hii kuongeza uzalishaji, kupanua mashamba yao, na kuinua kipato cha kaya,” amesema Mheshimiwa Hazali.
Mkuu wa Wilaya ya Hanang Mh. Almishi Hazali akikabidhi trekta kwa mkulima katika hafla ya mgao wa matrekta 20 yaliyotolewa kwa mkopo kupitia KANU Equipment na PASS Leasing.
Aidha, amewataka wakulima kuhakikisha wanatunza matrekta hayo kwa uangalifu na kuyatumia kwa shughuli za kilimo pekee ili manufaa yake yawe ya kudumu kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, CPA John Kajivo, amesema Halmashauri itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kama KANU Equipment na PASS Leasing ili kuhakikisha wakulima wanapata fursa za kifedha na zana za kisasa zinazorahisisha uzalishaji.
“Tumejifunza kuwa changamoto nyingi za kilimo zinatokana na upatikanaji wa zana na pembejeo kwa wakati. Kupitia ushirikiano huu, wakulima sasa wanapata suluhisho la uhakika,” amesema CPA Kajivo.
Naye Mkuu wa Idara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo Wilaya ya Hanang, Daniel Luther, amesema kati ya matrekta 20 yaliyokabidhiwa, 17 yamechukuliwa na wakulima wa ndani ya Hanang, jambo linalodhihirisha mwitikio chanya wa wakulima wa wilaya hiyo katika kutumia teknolojia za kisasa.
Ameongeza kuwa, kupitia kongamano la kilimo lililofanyika hivi karibuni, wakulima walipata fursa ya kujifunza kuhusu mbegu bora, mbolea za ruzuku, matumizi ya vishkwambi kwa maafisa ugani, na ujasiriamali wa kidijitali, hatua inayolenga kuifanya Hanang’ kuwa kitovu cha kilimo chenye tija nchini.
Serikali imeendelea kusisitiza kuwa, pamoja na upatikanaji wa zana za kisasa, wakulima wanapaswa kutumia maafisa ugani waliopo vijijini na vifaa vya kupima udongo vilivyotolewa, ili kuhakikisha kilimo kinakuwa na tija na kinachozingatia sayansi na teknolojia.
“Msingi wa mafanikio ya wakulima wetu ni kufanya kilimo cha kisasa, kinachotumia maarifa, teknolojia na ushirikiano na wadau,” amesema Luther.
Kupitia mgao huu wa matrekta, Wilaya ya Hanang’ inaendelea kuchukua nafasi muhimu katika utekelezaji wa ajenda ya serikali ya mapinduzi ya sekta ya kilimo (Agenda 10/30) inayolenga kuongeza tija, kipato, na usalama wa chakula kwa wananchi wote.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.