Katibu Tawala wa Wilaya ya Hanang, Mwalimu Athumani Likeyekeye, amesisitiza umuhimu wa nidhamu katika elimu na kuonya kuwa wazazi na walezi wanaochangia watoto wao kutohudhuria masomo kwa utoro watachukuliwa hatua za kisheria.
Ametoa onyo hilo alipohudhuria kama mgeni rasmi katika mahafali ya darasa la saba katika Shule ya Msingi Balangdalalu, ambapo alisisitiza kuwa jukumu la malezi ni la familia na linapaswa kushirikiana na walimu kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya elimu kikamilifu.
“Wazazi na walezi mnapaswa kufahamu kwamba elimu ndiyo nguzo ya maisha ya mtoto. Mnaposhirikiana na walimu, mnajenga taifa lenye misingi thabiti ya maendeleo. Utoro na kutelekeza wajibu wa malezi hakutavumiliwa, hatua za kisheria zitachukuliwa kwa atakayekiuka,” alisema Likeyekeye.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Teresia Irafay, aliwapongeza walimu kwa juhudi kubwa wanazofanya kila siku katika malezi na ufundishaji wa watoto. Alisema walimu ndio injini ya maendeleo ya taifa na mchango wao hauwezi kupuuzwa.
Aidha, aliwaasa wazazi na walezi kuhakikisha wanashirikiana kwa karibu na walimu katika safari ya elimu ya watoto wao, akibainisha kuwa mchango wao ni muhimu katika kuwalea na kuwajengea misingi imara ya kimaadili na kielimu.
“Elimu ni urithi bora zaidi ambao mzazi anaweza kumpa mtoto wake. Tunahitaji kushirikiana ili kuhakikisha kila mtoto anapata nafasi ya kujifunza, kukua na kuchangia maendeleo ya jamii na taifa letu,” alisema Irafay.
Kwa pamoja, viongozi hao walisisitiza kuwa nidhamu, mshikamano na ushirikiano kati ya walimu, wazazi na jamii kwa ujumla ndiyo msingi imara wa kuinua elimu katika Wilaya ya Hanang.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.