Wanawake wajasiriamali kutoka mkoa wa Manyara wamekutana mjini Katesh, Wilaya ya Hanang katika kongamano maalum la ufunguzi wa Jukwaa la Wanawake Wajasiriamali na kuwajengea uwezo, kukuza maarifa na kuwawezesha kiuchumi kupitia shughuli zao za kila siku za ujasiriamali.
Kongamano hilo limefanyika katika ukumbi wa Rode na limekusanya wanawake wa kada mbalimbali walioko katika biashara ndogondogo, viwanda vidogo, kilimo, usindikaji wa mazao na shughuli nyingine za uzalishaji mali.
Lengo kuu la jukwaa hilo ni kuwawezesha wanawake kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu bora za biashara na kufahamu fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia sera za serikali.
Mgeni rasmi katika ufunguzi wa kongamano hilo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Mheshimiwa Almishi Hazali, ambaye aliwahimiza wanawake kuondoa hofu na kuchangamkia kwa ujasiri fursa zilizopo kwenye sekta ya biashara na ujasiriamali.
"Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imejipanga kumuinua mwananchi kiuchumi kwa kuhakikisha kila mmoja anapata nafasi ya kushiriki kwenye maendeleo ya taifa. Hivyo basi, nawasihi wanawake kujiamini, kuanza pale walipo, hata kama ni kwa mtaji mdogo. Mnachotakiwa ni ujasiri, bidii na kufuatilia fursa zinazotolewa na serikali," alisema Mheshimiwa Hazali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Teresia Irafay, aliwahakikishia wanawake kuwa halmashauri inatambua mchango wao katika uchumi wa jamii na itaendelea kuwaunga mkono kwa vitendo. Alisema halmashauri imeendelea kutekeleza agizo la serikali la kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
"Hadi sasa tumeweza kutoa mikopo kwa vikundi vingi vya wanawake, na tutaendelea kuongeza juhudi kuhakikisha wanawake wengi zaidi wanafikiwa. Mikopo hii haina riba, na ni kwa ajili ya kuwawezesha kuanzisha au kukuza biashara zenu" alisema Irafay.
Kongamano hilo lilihusisha pia mafunzo ya kiutendaji, ushauri wa kibiashara, maonesho ya bidhaa zinazozalishwa na wanawake wajasiriamali, pamoja na vikao vya majadiliano kuhusu changamoto zinazowakabili wanawake katika sekta ya biashara.
Wanawake waliohudhuria waliishukuru serikali kwa kuwawezesha kupitia jukwaa hilo na kuahidi kutumia maarifa waliyopata katika kuendeleza miradi yao na kuinua kipato cha familia zao.
Kongamano hili linaendelea kuwa sehemu ya jitihada za kitaifa za kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika shughuli za maendeleo, huku Manyara ikiwa miongoni mwa mikoa inayotekeleza kwa vitendo mikakati ya kujenga uchumi jumuishi unaompa nafasi kila mwananchi.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.