Katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, wanawake wa Wilaya ya Hanang leo Machi 3, 2025 wameadhimisha siku hiyo kushiriki matendo ya huruma katika Hospitali ya Wilaya ya Hanang (Tumaini), kabla ya kuhudhuria kongamano kubwa lililofanyika katika Ukumbi wa Rhode, mjini Katesh.
Maadhimisho hayo yamebebwa na kauli mbiu ya mwaka huu: “Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji,” ikiangazia umuhimu wa kushirikiana katika kuleta maendeleo na kutetea haki za kijinsia.
Kabla ya kongamano, mamia ya wanawake waliandamana kwa amani wakibeba mabango yenye jumbe za kuhamasisha usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake, yaliyoanzia Hospitali ya Tumaini hadi Ukumbi wa Rhode na kupokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Mheshimiwa Almishi Hazali, ambaye alikuwa mgeni rasmi wa tukio hilo.
Katika hotuba yake kwenye kongamano hilo Mheshimiwa Hazali, aliwataka wanawake wa Hanang kutumia fursa zinazotolewa na serikali, ikiwemo mikopo isiyo na riba, ili kujiletea maendeleo.
"Wanawake wa Hanang mmekuwa na juhudi kubwa katika kujikwamua kiuchumi. Serikali itaendelea kuwaunga mkono kwa kuwapatia mikopo isiyo na riba kupitia halmashauri. Ni muhimu kutumia fedha hizo kwa nidhamu ili kujijenga kiuchumi," alisema Mheshimiwa Hazali.
Pamoja na kuhimiza maendeleo ya kiuchumi, Mheshimiwa Hazali alitoa wito kwa wanawake kuwa mstari wa mbele katika kupinga ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto, akiwataka wanawake kuacha kuwalinda wahalifu wa matukio hayo na badala yake kushirikiana na vyombo vya sheria kuhakikisha haki inatendeka.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, Gaudence William, alieleza kuwa katika mwaka wa fedha wa 2024/25, halmashauri imetenga ya shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya mikopo isiyo na riba kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu sasa, na hadi sasa zaidi ya shilingi milioni 500 zimekwishatolewa kwa vikundi mbalimbali vya wanawake.
"Lengo letu si tu kuwapa mikopo, bali kuwawezesha wanawake kufikia mafanikio makubwa ya kiuchumi. Tunataka kuona wanawake wa Hanang wanageuka kuwa mabilionea na wanatoa ajira kwa wengine," alisema William.
Katika kongamano hilo, wanawake walipata mafunzo kutoka kwa wataalamu wa sekta ya fedha, wakiwemo maafisa wa benki, ambao waliwapa mbinu za kutunza fedha, kukuza mitaji yao na kutumia rasilimali walizonazo kwa manufaa endelevu.
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake kwa Mkoa wa Manyara yanatarajiwa kufanyika Machi 5, 2025, katika Wilaya ya Mbulu, yakihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Queen Sendiga.
Kilele cha maadhimisho kitaifa kitafanyika Machi 8, 2025, jijini Arusha, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: 0787821459
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.