WASIMAMIZI wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Hanang wametakiwa kuhakikisha wanatoa ripoti sahihi za utekelezaji wa miradi tangu hatua za awali ili kuepusha changamoto wakati wa ukaguzi.
Akizungumza na walimu wakuu, watendaji, na wakuu wa idara mbalimbali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Teresia Irafay, alisisitiza kuwa uwazi na ufuatiliaji wa karibu wa miradi ni muhimu kwa mafanikio yake.
Aidha, amemtaka Mhandisi wa Halmashauri kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wasimamizi wa miradi ngazi ya chini kwa kuwapa ushauri wa kitaalamu bila vikwazo. Amesema tayari Serikali imemuwezesha mhandisi huyo usafiri, huku mpango wa kuongezewa gari lingine ukiwa mbioni ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yake.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Hanang, Mwalimu Athuman Likeyekeye, amepongeza hatua hiyo ya kuwaunganisha watendaji wa miradi, akisema kuwa ushirikiano wa karibu utaongeza ufanisi na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi hiyo.
"Miradi hii ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi wetu, na tunahitaji kuona kila mtu anawajibika ipasavyo. Ushirikiano wa karibu kati ya wasimamizi wa miradi, wahandisi, na uongozi wa halmashauri utahakikisha kuwa hakuna ucheleweshaji wala matumizi mabaya ya rasilimali," alisema Mwalimu Likeyekeye.
Aidha, alisisitiza kuwa miradi mingi ya maendeleo imekuwa ikicheleweshwa kutokana na changamoto za urasimu na ukosefu wa taarifa sahihi. "Ni muhimu kwa kila msimamizi wa mradi kutoa ripoti za utekelezaji kwa wakati na kwa usahihi ili kurahisisha ukaguzi na kuhakikisha fedha zinatumika kama ilivyokusudiwa," aliongeza.
Katika mwaka wa fedha 2024/25, Halmashauri ya Hanang inatekeleza miradi 105 katika sekta za Afya, Elimu, Kilimo, na Utawala. Mkurugenzi ameagiza miradi yote ikamilike kabla ya Mei 30, 2025, ili kuepusha ucheleweshaji wa maendeleo na kuzuia miradi viporo.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.