Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Dkt. Mohammed Kodi, ameongoza wataalamu kutoka Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Magonjwa Yasiyoambukiza inayoendelea kitaifa.

Akizungumza wakati wa utoaji wa elimu hiyo, Dkt. Kodi alisema lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu, kisukari, saratani, magonjwa ya moyo na magonjwa sugu ya njia ya hewa, ambayo kwa sasa yanaongezeka kwa kasi kimya kimya katika jamii.
“Tunawaelimisha wananchi kubadili mitindo ya maisha, kufanya mazoezi mara kwa mara, kupunguza matumizi ya sukari, chumvi na mafuta, pamoja na kuepuka uvutaji sigara na unywaji pombe kupita kiasi,” alisema Dkt. Kodi.
Elimu hiyo imetolewa kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Katesh pamoja na washiriki wa mikutano ya viongozi wa vijiji na kata, ambapo wananchi walipata nafasi ya kuuliza maswali na kupimwa afya zao bure.
Dkt. Kodi aliongeza kuwa wiki hiyo inalenga pia kuhamasisha uchunguzi wa mapema wa magonjwa yasiyoambukiza, kwani wagonjwa wengi hugundua wakiwa katika hatua za mwisho, jambo linaloongeza gharama za matibabu na kupunguza ufanisi wa tiba.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi na viongozi waliohudhuria elimu hiyo wamepongeza juhudi za wataalamu wa afya kwa kuwafikia moja kwa moja vijijini, wakisema elimu hiyo itasaidia kubadili mitazamo na tabia za wananchi kuhusu afya zao.
Wiki ya Magonjwa Yasiyoambukiza huadhimishwa kila mwaka nchini kwa lengo la kuhamasisha jamii kuishi kwa afya bora na kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa hayo, ambayo huchangia zaidi ya asilimia 30 ya vifo vinavyotokea nchini Tanzania kila mwaka.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.