Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ imeendelea kuwajengea uwezo watumishi wake katika nyanja ya upangaji na uandaaji wa bajeti kwa kutumia mfumo wa PLANREP (Planning of Revenue and Expenditure Projection), ili kuongeza ufanisi katika usimamizi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Mafunzo hayo yamefanyika kuanzia Oktoba 13 hadi 16, 2025, katika ukumbi wa Shule ya Msingi Katesh A, yakihusisha wakuu wa idara, vitengo, pamoja na maafisa watendaji wa kata na vijiji wote wa Wilaya ya Hanang’.
Awamu ya kwanza ya mafunzo ilihusisha wakuu wa vitengo na idara mbalimbali, ambapo Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Hanang CPA John Kajivo alifungua mafunzo hayo na kusisitiza umuhimu wa watumishi kuelewa kwa kina mchakato wa upangaji bajeti unaoendana na miongozo ya serikali, ili kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa tija na kwa wakati.
Awamu ya pili ya mafunzo, ilihusisha wasimamizi wa miradi ngazi ya kata na vijiji.
Akifunga mafunzo hayo leo Oktoba 16, 2025 Katibu Tawala wa Wilaya ya Hanang, Mwalimu Athumani Likeyekeye, ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliwataka washiriki kutumia ujuzi walioupata kuboresha upangaji wa miradi na matumizi sahihi ya fedha za umma katika maeneo yao.
Amesema serikali inaendelea kuimarisha uwezo wa watumishi katika ngazi zote za utawala ili kuhakikisha mipango ya maendeleo inaandaliwa kwa usahihi, inatekelezwa kwa wakati, na inatoa matokeo chanya kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Mipango, Erick Kayombo; mafunzo hayo ni sehemu ya mpango endelevu wa halmashauri wa kujenga uwezo wa watumishi katika matumizi ya mifumo ya kisasa ya serikali, ikiwa ni hatua muhimu katika kuboresha uwazi, uwajibikaji na ufanisi wa kiutendaji.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.