Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ imeanza kliniki maalum ya kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na watumishi walioko nje ya makao makuu ya halmashauri kama sehemu ya maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja duniani.
Kliniki hiyo, inalenga kusogeza huduma karibu na wananchi na kuimarisha mawasiliano kati ya serikali na jamii katika ngazi za vijiji na kata ambapo leo Oktoba 7, 2025 Afisa Utumishi wa Halmashauri, Martin Justine, ameongoza timu ya wataalam katika tarafa ya Endasaki, ambapo wananchi na watumishi mbalimbali walipata nafasi ya kueleza changamoto zao na kupatiwa majibu ya papo kwa papo kutoka kwa wataalamu husika.
Katika kliniki hiyo, wananchi wameeleza masuala yanayohusu huduma za kijamii, ajira, upandishaji vyeo, posho, upatikanaji wa taarifa za serikali, pamoja na ushirikishwaji katika miradi ya maendeleo. Wataalamu walihusika kutoa ufafanuzi, kushauri, na kuchukua hatua stahiki za kutatua changamoto hizo kwa wakati.
Aidha, watumishi wa sekta za afya, elimu, kilimo, na watendaji wa vijiji na kata walipata nafasi ya kusikilizwa kuhusu masuala ya kiutumishi, ambapo baadhi ya changamoto zao zilitatuliwa mara moja huku nyingine zikihifadhiwa kwa ufuatiliaji wa haraka.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Utumishi, Martin Justine, amesema kliniki hizo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’, Teresia Irafay, aliyetoa wito kwa watumishi wote kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi kama ishara ya uwajibikaji na uzalendo.
Kliniki hiyo itaendelea katika tarafa mbalimbali kwa ratiba ambapo kesho Oktoba 8, 2025 ni tarafa ya Bassotu, Balangdalalu ni Oktoba 9, 2025 kisha Simbay Oktoba 10, 2025 kabla ya kuhitimisha katika tarafa ya Katesh Oktoba 11, 2025
Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ imepanga kuendesha kliniki kama hizi mara kwa mara kama sehemu ya utekelezaji wa maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja, chini ya kauli mbiu ya "CHANGAMOTO YAKO NI WAJIBU WANGU" yenye lengo la kuongeza uwazi, ufanisi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma za umma.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.